- NINA mguu mmoja, mwingine umevunjika,
Kwa hatua moja moja, hivi ndivyo naondoka,
Ninajua siku moja, niendako nitafika,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Mbona hata huyo kobe, pole pole anafika,
Ni kwa nini unibebe, na wakati sijachoka,
Wewe nipigie debe, nivuke vyote vichaka,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Unajua sitembei, bali ninarukaruka,
Teso langu siombei, na wewe likakufika,
Wala mimi siongei, kama nimefilisika,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Moja yangu pia bora, namshukuru Rabuka,
Nisijepigiwa kura, kwamba ninalalamika,
Mwenyewe akunje sura, na huo ajenipoka,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Nitakuja piga nduru, mwisho nitakapofika,
Hata kama ni Tunduru, kelele zitasikika,
Kwamba nimeona nuru, kileleni nimefika,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Wapo wanaodhania, kwamba ninafadhaika,
Tena wanafikiria, guu moja litachoka,
Waijue yangu nia, ni kileleni kufika,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Badala ya kushangaa, na yangu kuhangaika,
Hebu cheki yako saa, muda wako wakatika,
Fanya yanayokufaa, pazuri yatakuweka,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Wa mbili havai moja, msemo unasikika,
Lakini naye wa moja, anapaswa kutamka,
Kwamba anaweza kuja, hata kwa kuchoka choka,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Nasema na wangu moyo, nje hayatasikika,
Usijevunjika moyo, kimoja kikikutoka,
Jua Mungu huyo huyo, hatakuacha hakika,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Miye mbele ninasonga, njiani sitadondoka,
Na mlango nitagonga, pasipo hata kuchoka,
Na maombi nitachonga, hadi nitaposikika,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Mungu wetu anajua, sisi tukihangaika,
Mizigo kwake kitua, atatupa ushirika,
Na siku tusoijua, tutakuja changamka,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Ndugu sikate tamaa, yale mambo umeshika,
Hata yawe ni balaa, yanayoleta kuchoka,
Mungu atayavagaa, na yote yatayeyuka,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Hata kama ni maombi, ya kuzitaka baraka,
Wewe usifanye dhambi, kwa Mungu zidi kudeka,
Kwako atapiga kambi, na kukujibu haraka,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Mwenye miguu miwili, hiyo kwako ni baraka,
Situmie kikatili, wengine ukawacheka,
Yatakukuta makali, ubaki kubabaika,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Ona wale makatili, jinsi wanavyoumbuka,
Yabumbuluka madili, na kuvileta vibweka,
Mwisho wakata kauli, watupwa kwenye machaka,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Ukiikosa busara, na kuuvuka mpaka,
Asoangalia sura, kifungoni takusweka,
Na huko tutakuchora, kama zile takataka,
Japo mguu mmoja niendako nitafika - Mungu wangu niongoze, njia ninayoishika,
Lengo nikalitimize, hata ipite miaka,
Wengi wakajiulize, ni kwa vipi nimefika,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika. - Hata sasa Bwana Mungu, umenibeba hakika,
Hata kikija kiwingu, wala sitafadhaika,
Ninajua ndani yangu, katu sitajaumbuka,
Japo mguu mmoja, niendako nitafika.
Na Lwaga Mwambande
lwagha@gmail.com (KiMPAB) 0767223602