- KUANGUKA sio tatizo, hata ukifika chini,
Ni sawa sawa na nguzo, iliyokuwa angani,
Lazima vuta uwezo, kuirudisha mbinguni,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini. - Inuka jishikilie, sio kwako hapo chini,
Usikae utulie, unachelewa kazini,
Jinyanyue jiambie, siyo pako hapo chini.
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini. - Wewe nguzo ya umeme, juu kwa juu safarini,
Nyaya chini ni kiwewe, ni hatari duniani,
Ziwe juu kwenye mwewe, kote ibaki amani,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini. - Watu wengi huanguka, wanapokuwa njiani,
Hawabaki wakadeka, kusalia pale chini,
Hutafuta cha kushika, kuinuka toka chini,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini. - Tena unapoanguka, iingie akilini,
Sababu ya kuanguka, isirudie njiani,
Dalili ukizinyaka, unakwepea pembeni,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini. - Kuanguka si habari, igusayo sikioni,
Kuinuka ni habari, sote tunaitamani,
Wachungulia kaburi, unarudi ahueni,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini. - Maisha ni kuinuka, hata kuanguka chini,
Hatubaki kubweteka, kuloa chozi shavuni,
Hung’ang’ana kuinuka, kupambana duniani,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini. - Biashara uloshika, mtaji u mavumbini,
Jipigepige inuka, uingie mzigoni,
Ya jana hayatanuka, kesho ndio i njiani,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini. - Wengi wanaosikika, walishuka hadi chini,
Wababe waliwachoka, wakasogea pembeni,
Hao walichangamka, hawakusalia chini,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini. - Bill Gates asikika, tajiri wa duniani,
Shuleni hakutukuka, kama wale kilingeni,
Sasa wasomi ateka, kawaajiri kazini,
Kuanguka we anguka, ila usibaki chini.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)