NA MAGENDELA HAMISI,DAR ES SALAAM
TANZANIA na Cuba wamekubaliana kushirikiana katika nyanja ya kilimo, afya , utalii na elimu na kusaini hati za makubaliano ambayo ni sehemu ya kudumisha uhusiano wa mataifa hayo ambao umedumu tangu mwaka 1962 chini ya wahasisi wa nchi hizo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Fidel Castrol.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaama leo, Januari 24, 2024 ametanabaisha kuwa katika upande wa afya watahakikisha kiwanda cha dawa cha TBPL kilichopo Kibaha mkoani Pwani ambapo ni cha kipee barani Afrika kinajengewa uwezo ili kilete mafanikio yanayohitajika.
Ameongeza mchakato ya kukijengea uwezo kiwanda hicho kinakwenda sanjari na kushirikiana katika utafutaji wa masoko ili kuimarisha uchumi.
Kiwanda hicho cha kutengeneza viuadudu kinamilikiwa kwa asilimia mia moja na Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo (NDC) kikiwa ni mahusus katika kupambana na malaria na kina uwezo wa kuzalisha lita milioni sita kwa mwaka na ujenzi wake ni matokeo ya ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Cuba.
Pia katika mazungumzo ya leo Januari 24,2024 , Dk Mpango amebainisha kuwa Cuba, wamekubali kuongeza watalaam wa afya kwa upande Tanzania Bara na Zanzibar.
Dk.Mpango amesema baada ya kufanya mazungumzo kwa kina leo asubuhi, pia wamekubaliana kushirikiana katika nyanja ya siasa jambo ambalo ni mkakati madhubuti kwenye kujiimalisha katika medani ya siasa.
“Nashukuru kuona baada ya kufanya mazungumzo na ndugu zetu hawa pia wameonesha nia ya dhati katika kukitangaza Kiswahili nchini mwao jambo nasi tutawaunga mkono katika hilo ili kufanikisha ndoto za kueneza lugha ya Kiswahili katika mataifa mengine,” amesema.
Naye Makamu wa Rais wa Cuba, Salvador Valdés Mesa ameishukuru Tanzania kwa kuwa mstari mbele kuzungumzia suala la vikwazo vya kiuchumi, biashara na kifedha (Broken)ambavyo ni hiyo wamewekewa ingawa wanapambana kuhakikisha wanasimama imara.
Akizungumzia kuhusu kusainiwa hati za makubaliano amesema kuwa wataendelea kudumisha uhusiano ulipo kupita sekta mbalimbali ikiwemo ya afya mchakato utakaosaidia Tanzania kupata dawa zenye viwango vya juu kutoka nchini Cuba.
Hati hizo za makubaliano zimesainiwa kati ya Chuo Kikuu cha Atemisa cha Cuba na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Tanzania katika lengo lake likiwa kufanikisha nyanja ya kilimo inakuwa madhubuti na kwa upande wa ushirikiano kwenye nyanja ya afya Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa na Vifaa Tiba ya Serikali ya Cuba (CECMED) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ya Tanzania (TMDA) zilisaini hati ya Makubalina kushirikiana katika nyanja hiyo.