WAZIRI wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, ameushauri uongozi wa Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Anglo Gold Ashanti, inayomiliki Mgodi wa Dhahabu wa Geita (Geita Gold Mine-GGM), kuanza kuiuzia Serikali dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania ili kuiwezesha Serikali kuhifadhi dhahabu kama akiba ya fedha za kigeni. Dk. Nchemba ametoa ushauri huo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Ofisa Mkuu wa masuala ya Fedha wa Kampuni hiyo, Gillian Doran, ambapo wamejadili masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya Kampuni hiyo na Serikali. Amesema kuwa hatua hiyo itaifanya Serikali kuwa na chanzo cha uhakika cha kupata dhahabu pamoja na kuwatumia wachimbaji wadogo ambao hivi sasa ndio wanaofanyabiashara ya kuiuzia dhahabu Benki Kuu ya Tanzania. “Lengo la hatua ya Serikali ya kuanza kuhifadhi dhahabu kama fedha za kigeni ni kuifanya nchi kuwa na chanzo cha uhakika cha fedha za kigeni kitakachotumika kama dhamana wakati inapohitaji fedha hizo kwa ajili ya matumizi mbalimbali badala ya kutegemea mikopo” amesema Dk Nchemba. Aidha, Dk. Nchemba amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameilekeza Wizara ya Fedha kuanza kununua dhahabu na kuitunza kama fedha za kigeni, maelekezo ambayo tumeyatekeleza na Benki Kuu imeanza kununua dhahabu. “Akiba ya Dhahabu itatusaidia kununua bidhaa muhimu zitakazokuwa zinahitajika nchini ikiwemo mafuta na bidhaa nyingine, wakati wa changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni na hatua hii inafaida kubwa kiuchumi” amesisitiza Dk Nchemba Vilevile Dk. Nchemba amesema kuwa mitambo ya kuchenjua dhahabu iliyojengwa Geita na Mwanza, itakuwa na manufaa endapo dhahabu inayozalishwa nchini itachakatwa na kuongezwa thamani hapa hapa nchini na kuchangia pato la Taifa. Katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imejipanga kununua tani sita za dhahabu kwa ajili ya kuweka akiba katika mfumo wa fedha za kigeni. Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa masuala ya Fedha wa Kampuni ya Anglo Gold Ashanti, Doran, ameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara na kuahidi kuwa itaimarisha zaidi ushirikiano na Serikali kupanua uzalishaji wa madini nchini. Ameahidi kuufanyia kazi ushauri uliotolewa wa kuiuzia Serikali dhahabu kama njia ya kutunza fedha za kigeni lakini pia kuendelea kusaidia huduma za kijamii katika aneo la mgodi wa dhahabu wa Geita kwa manufaa ya wananchi.