NA MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko,
ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dk
Samia Suluhu Hassan imeamua kwa dhati kuwekeza katika miradi ya
nishati nchini huku lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa upatikanaji umeme
nchini unakuwa mkubwa kuliko mahitaji ya nchi.
Amesema hayo leo Januari 18, 2024 jijini Dodoma wakati Wizara ya
Nishati ilipowasilisha taarifa kuhusu hali ya uzalishaji na usambazaji
umeme nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Kikao
ambacho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga,
Katibu Mkuu, Mhandisi, Felchesmi Mramba, baadhi ya Wakuu wa Taasisi
zilizo chini ya Wizara na Watendaji wa Wizara ya Nishati.
“ Moja ya vipaumbele vikubwa vya Serikali ni Sekta hii ya Nishati na
ndio maana fedha zimekuwa zikitolewa za kutekeleza miradi mbalimbali
ya Nishati ikiwemo mradi mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP)
ambao gharama yake ni Sh. Trilioni 6.5 na hadi sasa Serikali
imeshamlipa mkandarasi shilingi Trilioni 5.7 ambayo ni sawa na asilimi
88.7.” amesema Dk.Biteko
Kuhusu usimamizi wa mradi wa JNHPP amesema kuwa, Serikali iko makini
katika usimamizi wake na kwamba kuna mamlaka mbalimbali zinazosimamia
mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa ufanisi akitolea mfano Timu
Maalumu ya Wataalamu iliyoundwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya
kusimamia mradi huo ambayo inaongozwa na Profesa Idris Kikula.
Kuhusu hali ya miundombinu ya umeme nchini, Dk. Biteko amesema kuwa,
itaendelea kufanyiwa matengenezo ili iweze kuzalisha, kusafirisha na
kusambaza umeme kwa ukamilifu wake, huku juhudi za kujenga miundombinu
mingine upya ikiendelea.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga
alieleza Kamati kuwa, mradi wa umeme wa JNHPP kwa sasa umefikia
asilimia 95.8 na kwamba mtambo namba Tisa utakaozalisha megawati 235
umeshakamilika na mtambo Namba 8 na namba 7 ipo mbioni kukamilika.
Kuhusu hali ya umeme nchini, Mhandisi Nyamo-Hanga amesema kuwa, pamoja
na jitihada mbalimbali zinazoedelea kufanywa na Serikali ili kupunguza
changamoto ya umeme nchini, hali ya upungufu wa umeme itaisha mara
baada ya kuwashwa kwa kwa mashine mbili za JNHPP zenye uwezo wa
megawati 470 ambazo zinatarajiwa kuwashwa kabla ya mwezi Machi, 2024.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini, Dk. David Mathayo David pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo
wamepongeza viongozi wa Wizara ya Nishati kwa usimamizi mzuri wa
Sekta na kueleza kuwa wana imani kwamba viongozi hao kwa kushirikiana
na Taasisi zake wataiwezasha nchi kuwa na Nishati ya kutosha, ya
uhakika na inayotabirika.