NA TERESIA MHAGAMA,ZANZIBAR
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ametoa
wito kwa Wananchi kuendelea kuyaenzi, kuyalinda na kuyaishi kwa
dhamira ya dhati, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwani Waasisi wa Nchi
walifanya mapinduzi hayo ili kuwa na Taifa huru ambalo kila mtu
anakuwa na hadhi, kuondoa dhuluma iliyokuwepo na kufanya wananchi
kuishi kwa amani na furaha.
Amesema hayo Leo Januari 6,2024 wakati akizungumza na Wananchi
katika Wilaya ya Mkoani, mkoani Kusini Pemba mara baada ya kuzindua
Afisi ya Uhamiaji na Makaazi ya Askari wilayani humo.
“ Sisi Wananchi tunawajibu wa kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar
kwa kuyaishi, kuyaheshimu, kukuza uchumi wa nchi na kukuza uzalendo
ili baada ya muda mrefu hata baada ya miaka 100 mbele, watakaokuja
kusherehekea Mapinduzi haya wakute Zanzibar iliyobora zaidi na waseme
Mapinduzi haya yalitufaa.” amesema Dk Biteko
Ameeleza kuwa, moja ya tunu tuliyonayo ni mshikamano hivyo watu
wasiruhusu mtu yoyote kuwagawanya kwa misingi yoyote ile, bali
maendeleo yaunganishe watu wote na kwamba tofauti za vyama, dini na
kabila visifanye watu wakae kwenye makundi bali kuunganisha watu kwa
maslahi ya nchi na watanzania.
Amesema kuwa, nchi inapoenda kusherehekea Siku ya Mapinduzi ya
Zanzibar tarehe 12 Januari mwaka huu, watanzania wote waungane
kuwaombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk, Samia Suluhu
Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, ili waendelee
kuongoza vyema, kuimarisha ustawi wa Taifa na kuwaunganisha
Watanzania.
Kuhusu Jengo hilo jipya la Afisi ya Uhamiaji katika Wilaya ya Mkoani,
mkoani Kusini Pemba, Dk. Biteko amesema kuwa ni moja ya matunda ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwani kabla ya Mapinduzi watu
walinyimwa haki zao za kimsingi zikiwemo za uhamiaji kama vile kupata
pasi ya kusafiria na hivyo Mapinduzi yamewezesha wananchi kupata uhuru
wa kusafiri nje ya mipaka ya nchi.
Ameongeza kuwa, Ofisi hiyo ya Uhamiaji wilaya ya Mkoani ilianza mwaka
1979 ikiwa ni ndogo lakini sasa kuna jengo la kisasa litakalowezesha
upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wa Wilaya hiyo na viunga
vyake, ikiwa ni kielelezo cha Mafanikio ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amepongeza viongozi Wakuu wa nchi kwa juhudi wanazochukua ili wananchi
wapate huduma bora ikiwa pia ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha
Mapinduzi.
Vilevile amewapongeza viongozi wa Idara ya Uhamiaji kwa usimamizi wa
jengo hilo na kuiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuona namna
ya kujenga jengo kama hilo katika wilaya mbalimbali nchini kwani ni
jengo la kisasa lililozingatia watu wenye mahitaji maalum, limechukua
eneo dogo na kujengwa kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne
Sagini amemshukuru Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mambo mema
anayoyafanya kwa kwa vyombo vya usalama nchini ikiwemo kutoa vibali
vya ajira, upandishaji vyeo, mafunzo, ulipaji madeni na kuwezesha
vyombo vya usalama kwa kununua vitendea kazi.
Amesema kuwa, Idara ya Uhamiaji imeendelea kufanya vizuri katika
ukusanyaji wa mapato yanayotokana na Idara hiyo kwani mwaka 2022/2023,
Idara ililenga kukusanya shilingi bilioni 56.5 lakini ilifanikiwa
kukusanya Sh.Bilioni 67.679 na mwaka huu wa fedha unaoendelea
imekusudia kukusanya shilingi bilioni 75 lakini hadi mwezi Desemba
ilikusanya bilioni 43.119 ambayo ni zaidi ya nusu ya malengo huku
matarajio yakiwa ni kufikia malengo yaliyowekwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk
Islam Seif, amesema kuwa, Afisi hiyo ya uhamiaji ilianza kujengwa
mwezi Agosti mwaka 2022 na kukamilika mwezi Novemba, 2023 huku akisema
kuwa jengo hilo la kisasa litakidhi mahitaji ya sasa ikiwemo uwepo wa
mifumo ya Tehama ambayo ni muhimu katika ufanyaji katika afisi hizo.
Amesema gharama za ujenzi wa Afisi hizo ni Sh. Bilioni 1 na
milioni 53 huku akieleza kuwa jengo lililopo linaakisi gharama hizo.
Amemshukuru Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi kwa kuendelea
kutekeleza miradi ya kimkakati Pemba ikiwemo kujenga uwanja wa ndege
wa kimataifa, mahoteli pamoja na afisi za kisasa.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala
amemshukuru Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein
Ali Mwinyi kwa kuboresha maslahi ya wafanyakazi na pia kuboresha
huduma mbalimbali za wananchi.
Amesema kuwa mafanikio mbalimbali yanayotokea sasa ni kutokana na
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyofanyika mwaka 1964 ambapo pia
Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar uliasisiwa.
Amesema Idara hiyo inaendelea na ujenzi wa jengo jingine la Afisi
katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo amepongeza Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kwa kutoa maeneo ya ujenzi wa Afisi hizo.