DAR ES SALAAM, TANZANIA
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu leo amezindua Programu ya Binti Mzalendo iliyoandaliwa na Ngome ya Vijana Mkoa wa Dar es salaam kwa ajili ya kuwatambua, kuwavutia, kuwahamasisha na kuwalea kiuongozi Mabinti katika Chama cha ACT Wazalendo.
Ndugu Ado Shaibu ameupongeza uongozi wa Ngome ya Vijana Mkoa wa Dar es salaam kwa ubunifu wao ambao amesema utasaidia kuwavutia Mabinti wengi kushiriki katika nafasi za uongozi ndani ya Chama na kwenye vyombo vingine vya maamuzi.
Ndugu Ado amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa ushiriki wa mabinti na wanawake kwa ujumla kwenye nafasi za kiuongozi kwenye vyombo vya maamuzi bado ni mdogo.
“Mathalani, katika uchaguzi mkuu uliopita, takwimu zinaonesha kuwa wagombea ubunge wanawake walikuwa 9.2% peke yake nchi nzima” alisisitiza Shaibu.
Ndugu Ado alisisitiza kuwa katika kurekebisha hali hiyo ni lazima vyama vibadilike kisheria, kisera na kiutamaduni. “Vyama vya Siasa haviwezi kuzungumzia usawa wa kijinsia kama vyenyewe havitaki kubadilika na vinakumbatia mfumo dume. Kabla ya kuibadili nchi, sisi wenyewe wanasiasa ni lazima tubadilike” alisisitiza Shaibu.
“Sisi ACT Wazalendo tumekuwa tukichukua hatua kiasi. Ukitazama kuanzia ngazi ya viongozi wakuu, wajumbe wa Kamati Kuu wa Kuchaguliwa, Wajumbe wa Halmashauri Kuu wa Kuchaguliwa, Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini na vitengo vingine vina wanawake wengi” aliongeza Shaibu.
“Hata hivyo hatua hiyo haitoshi. Kamati Kuu imeagiza sasa ni lazima Chama kiwe na Sera ya Jinsia kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa maradufu zaidi”
Katibu Mkuu Ado Shaibu amesema mpango wa Binti Mzalendo chini ya uongozi wa Ngome ya Vijana Mkoa wa Dar es salaam utakuwa chachu ya kuongeza ushiriki wa mabinti wengi waliotimiza miaka 18 na kuendelea kwenye siasa ndani ya Chama cha ACT Wazalendo