NA DANSON KAIJAGE,DODOMA
HATIMAYE Kata ya Kilimani katika Jiji la Dodoma imeanza ujenzi wa shule ya msingi itakayogharimu kiasi cha sh.milioni 80 kwa kuanza na vyumba vinne vya madarasa.
Ujenzi huo wa shule ya Msingi unatokana na Kata hiyo kutokuwa na shule ya msingi wala Sekondari tangu kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika na sasa ni Tanzania.
Kutokana na kutokuwa na shule katika kata hiyo licha ya kuwa na uongozi wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM),ilisababisha watoto kutembea umbali wa zaidi ya kilometa tatu kwa ajili ya kwenda kwenye shule za jirani.
Oktoba 11, 2023 Viongozi wa Kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi Kata ya Kilimani Jijini Dodoma pamoja na Wajumbe wa Sekretarieti ya Kata ya Kilimani wamefnya ziara ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa Shule ya Msingi unaotekelezwa katika Mtaa wa Chinyoyo Kata ya kilimani na kuridhishwa na utekelezaji wake.
Pamoja na kasi ya ujenzi huo unavyoendelea viongozi hao wamesisitiza ujenzi huo uongezewe kasi ili ukamilike kwa haraka na kwa wakati.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Kilimani,Nathan Chibeye amesema ujenzi huo wa shule ya Msingi utakuwa mkombozi kwa Kata hiyo na kuondoa adha ya watoto kutembea umbali mrefu kwenda shule za jirani.
“Kwa kuwa Kata hii tangu ipate Uhuru haijawahi kuwa na Shule ya Msingi jambo ambalo hupelekea watoto wa mitaa yote minne ya kilimani kusoma katika shule za kata nyingine na kusababisha kutembea umbali mrefu kuitafuta elimu sasa changamoto hiyo itakuwa imekwisha pale ujenzi utakapokuwa umekamilika” amesema
Licha ya hayo amesema wao kama viongozi wa CCM Kata ya Kilimani wanaishukuru Serikali ya awamu sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuwapatia fedha za ujenzi wa shule hiyo ambayo itakuwa mkombozi kwa wananchi wa kata ya kilimani.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Kata ya Kilimani Rotta Ndimbo ameitaka kamati ya ujenzi na Mkandarasi kuhakikisha wanatanguliza uzalendo katika ujenzi wa shule hiyo ili thamani ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi huo zinatumika kama zilivyo kusudiwa.
Ziara hiyo ya viongozi wa CCM Kata ya Kilimani ni mwendelezo wa kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali katika kata hiyo ili kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Chama unafanikiwa.