NA WAANDISHI WETU, SONGEA
NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameibeba kwa dhati ajenda ya matumizi ya nishati mbadala kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
Kapinga amesema hayo Oktoba 5, 2023 wakati wa Baraza Maalum la Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Ruvuma, sanjari na ugawaji wa majiko/mitungi ya gesi iliyotolewa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
“Ninyi nyote mnafahamu ajenda ya Mhe. Rais kuhusiana na umuhimu wa nishati mbadala, tunafahamu changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na changamoto za mazingira kwa ujumla. Hii ni ajenda ambayo Mhe. Rais ameibeba kwa dhati kabisa kuhakikisha tunaanza mchakato wa kuelimisha Watanzania ili kuondokana na nishati ambazo sio rafiki kwa mazingira, na kutumia zilizo rafiki kwa mazingira,” amesema Kapinga.
Naibu Waziri Kapinga ambaye pia ni Mbunge wa Vijana Mkoa wa Ruvuma amewataka vijana kushirikiana na wanawake, wazee na makundi mengine katika kuhakikisha wanapunguza changamoto za kimazingira kwa matumizi ya nishati mbadala.
“Wengi wanadhani ajenda hii ya nishati mbadala ni kwa ajili ya akina mama tu, lakini wote tunafahamu nguvu na mchango wa vijana kwenye masuala ya mabadiliko chanya. Kwa hiyo ajenda hii ni lazima twende nayo pamoja wanawake, vijana, wazee na kila kundi kwenye jamii. Ndiyo maana nikaona busara kushirikisha Baraza la Mkoa kwa sababu ninyi ndio viongozi kwenye Wilaya zenu,” amesema Kapinga.
Akifafanua, amesema kuwa ajenda ya matumizi ya nishati mbadala ni ya Serikali ya Awamu ya Sita na inatakiwa kuungwa mkono na wananchi wote ili kuweza kuboresha mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea hivi sasa duniani kote.
Kapinga amesema ni wakati wa vijana kusaidia katika anjenda mbalimbali zenye manufaa ya taifa na kwamba ajenda ya nishati mbadala ikibebwa na vijana inaweza kwenda kwa kasi katika kusaidia kupunguza changamoto za uharibifu wa mazingira unaofanywa na jamii.
Aidha, ameongeza kuwa wakati huu ambapo REA wanaendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati mbadala, Mhe. Rais ametoa mitungi ya gesi kwa Wabunge wote ili iende kwenye maeneo yote, na majimbo yote ili kuhamasisha umuhimu wa nishati mbadala.
Awali, akiwasilisha Mada kuhusu nishati safi ya kupikia, Mhandisi Kelvin Tarimo kutoka REA amesema Wakala hiyo inaendeshwa kwa Mipango Mikuu mitatu ambayo ni Mpango wa Sera ya Taifa wa Upelekaji Nishati Vijijini (Rural Energy Master Plan), Mpango wa usambazaji wa huduma ya umeme vijijini (Rural Electrification Master Plan) pamoja na Mpango wa Nishati safi za kupikia.
Kuhusu Mpango wa nishati safi ya kupikia, Mhandisi Tarimo amesema umelenga kuhamasisha matumizi ya nishati iliyo salama kwa mtumiaji na kwa mazingira, ubora, upatikanaji wake, gharama nafuu, rafiki kwa mazingira na iliyo endelevu.
Akizungumzia aina za nishati za kupikia na kiwango cha matumizi yake kwa hapa nchini, Mhandisi Tarimo amebainisha kuwa kuni inaongoza kwa asilimia 63. 5 ikifuatiwa na mkaa asilimia 26.2, gesi oevu asilimia 5.1, umeme asilimia 3 na asilimia 2.2 vyanzo vinginevyo.
Amesema, kutokana na matumizi makubwa ya mkaa na kuni, imechangia uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na ukataji miti. Pia, amesema athari nyingine ni za kiafya kwa watumiaji wa nishati hizo ambapo vifo zaidi ya 33,000 hutokea kwa mwaka kutokana na kuvuta hewa ya ukaa. Vilevile, kiuchumi amesema matumizi ya nishati zisizo salama yanachelewesha maendeleo ya shughuli za kiuchumi.
Kufuatia hali hiyo, amesema Serikali imeweka mikakati ya makusudi katika kuelimisha na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala hivyo akatoa wito kwa wananchi wanaopata elimu hiyo kuifikisha kwa wengine.
Amewasihi wananchi kubadili mitazamo hasi dhidi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo imani kwa baadhi ya watu kwamba chakula huwa kitamu zaidi kikipikwa kwa kutumia mkaa au kuni kuliko kikipikwa katika jiko la gesi au umeme.
Mhandisi Tarimo ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono kampeni ya Mheshimiwa Rais kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Naibu Waziri Kapinga yuko katika ziara ya kazi mkoani Ruvuma kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati pamoja na kuzungumza na wananchi.