NA MWANDISHI WETU, IRINGA
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umesema utahakikisha unashirikiana na
sekta binafsi katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na nishati
ya uhakika vijijini.
Mkurugenzi waTeknolojia za Nishati Jadidifu na Nishati Mbadala wa REA, Mhandisi Advera Mwijage alisema hayo baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa
umeme wa maji (kilovoti 2400) wa Idete wilayani Kilolo unaotekelezwa na Kampuni ya Lung’ali
Natural Resources Co ltd.
Amesema hadi sasa REA imedhatoa ruzuku ya Sh.Bilioni 4 kwa mradi huo
ulio chini ya Kanisa Katoliki mkoani Iringa ambazo zimetumika kwa
utafiti wa mazingira, ujenzi wa bomba la maji na jengo lenye mtambo wa kuzalishia umeme (Power House).
Pia, amesema REA ina wajibu wa kuwaunganisha wazalishaji wadogo na
taasisi zinazotoa mikopo kwa riba nafuu ambapo Benki ya TIB imeikopesha
kampuni hiyo ili ikamilishe mradi huo wa umeme kwa wakati na kuingiza kwenye gridi ya taifa.
“REA inafanya kazi na sekta binafsi katika kuhakikisha
upatikanaji wa huduma bora ya nishati vijijini na kuchangia katika
shughuli za uchumi zinazoongeza kipato kwa wananchi,” alisema Mhandisi Mwijage.
Aliongeza kuwa serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu hasa
katika miradi ya maendeleo inayogusa wananchi na hivyo kutambua
umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi.
Serikali imekuwa ikiipatia REA fedha ili kuwawezesha kufadhili miradi
ya wazalishaji wadogo binafsi wa umeme ili miradi hiyo ichangie katika kiasi cha umeme
kinachozalishwa katika gridi ya taifa .
Mhandisi Mwijage ameweka wazi umuhimu wa wazalishaji wadogo wa umeme, katika
maendeleo ya wananchi, na kusema serikali itaendelea kushirikiana nao.
Akieleza zaidi, amesema kuwa miradi ya uzalishaji umeme wa maji inasaidia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na inatunza mazingira hasa kwa kuwezesha kuachana na matumizi ya jenerata katika kuzalisha umeme.
“Miradi hii pia inaiongezea serikali kipato kwa kulipa kodi, kuzalisha
ajira na kuwapa wananchi uhakika wa upatikanaji wa umeme na hivyo
kushiriki kikamilifu katika shughuli za kujiongezea kipato,” alisema
Mkurugenzi wa Nishati Mbadala na Teknolojia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni inayozalisha umeme huo wa
maji, Lung’ali Natural Resources, Padre Luciano Mpoma alisema
wanatarajia kuanza uzalishaji wa umeme Januari mwakani na kwamba ujenzi
unaendelea vizuri.
Mradi huo utakapokamilika amesema wananchi wa Idete na maeneo mengine
watakuwa na umeme wa uhakika na hivyo kuweza kushiriki kikamilifu
katika shughuli za kiuchumi na huduma za kijamii.
Naye Mwenyekiti wa Kata ya Kidete, Henry Kikoti ameelezea shauku ya
wananchi kutaka mradi huo ukamilike kwani utaenda kuwa suluhu kwa
umeme wa uhakika kwani uliopo hautoshelezi mahitaji ya shughuli za
kiuchumi hasa kutokana na maendeleo na uwekezaji wa wananchi katika
nyanja mbalimbali za kiuchumi.