NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MWANAHARAKATI Deusdedith Soka, ameliandikia Jeshi la Polisi la nchi hiyo barua ya kutaarifu kuwa anataka kuandamana kupinga Serikali ya Tanzania kuingia kwenye mkataba na Serikali ya Dubai ya kuendesha bandari za nchi hiyo iliyopo Afrika Mashariki.
Demokrasia ilifanikiwa kuiona barua hiyo aliyoiandika Juni 15, 2023 kwenda kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
“Nikiwa kama raia wa Tanzania, nimepanga kufanya maandamano nikitokea nyumbani kwangu Temeke Juni 19, 2023 Saa 4:00 asubuhi kuelekea Ikulu ya Magogoni na kutoa taarifa kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuachana kabisa na utiaji saini muswada wa TISS,” ilisema barua hiyo iliyoandikwa na Soka
“Vilevile kwenye mkataba wa DP World (wa ubinafsishaji wa bandari), utazamwe upya na Rais Samia asitishe mkataba huo unaoonesha hauna kikomo.” aliandika Deusdedith kwenye barua hiyo.
Mwanaharakati huyo leo ameandika kwenye mtandao wa kijamii akieleza kuwa ameitwa kituo cha Polisi cha Temeke ili akachukue majibu yake.
“Nimepigiwa Simu na mkuu wa kituo cha Polisi #TMK akinitaka niende kuchukua
Majibu baada ya mabishano kwamba sehemu niliyopeleka barua ni sahihi.
Sijui kitakachotokea kwa upande wangu nitakapofika kituoni hapo. Ila nipo tayari kwa lolote. Jukumu la kulinda nchi ni letu” aliandika Deusdedith kwenye akaunti yake ya mtandao mmoja wa kijamii.
Mjadala umezuka kwenye mitandao ta kijamii nchini Tanzania baada ya kuonekana kwa mkataba wa makubaliano ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai wa kutaka kushirikiana kuziendesha bandari za Tanzania bara
Bunge la nchi hiyo, Jumamosi, Juni 10, 2023 iliridhia serikali ya nchi hiyo kuingia kwenye mkataba na Dubai wa kuendesha bandari.