NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KATIKA kuelekea Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu, Benki ya CRDB imezindua promosheni ya “Timiza Ndoto yake na Junior Jumbo” ikiwa na lengo la kuwahamasisha wazazi/ walezi juu ya umuhimu wa kuwawekea watoto wao akiba.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Meneja Mwandamizi wa Mauzo, Muhumuliza Buberwa amesema kupitia kampeni hiyo Benki ya CRDB pia imejipanga kutoa elimu ya fedha kwa watoto ili kuanza kuwaandaa mapema kukabiliana na changamoto za kifedha. “Tumekuwa tukiwafundisha watoto juu ya mambo mbalimbali katika maisha, lakini watoto walio wengi wanakosa elimu juu ya fedha na kujiwekea akiba, elimu ambayo ni muhimu sana kwa watoto na vijana wetu.
Kampeni hii inakwenda kuhimiza juu ya ya umuhimu wa elimu, pamoja na kuwafundisha watoto kujenga utamaduni wa kuanza kujiwekea akiba,” amesema Buberwa.
Akielezea kuhusu muda wa kampeni hiyo Meneja Mauzo wa Benki ya CRDB, Amina Mawona amesema katika promosheni hiyo ya “Timiza Ndoto yake na Junior Jumbo” ambayo inatarajiwa kufikia kikomo Julai 5, 2023, Benki ya CRDB imetenga kiasi cha shilingi milioni 15.4 kama zawadi ya ada kwa ajili ya watoto 21 ambapo kila kanda ya benki hiyo kunatarajiwa kuwa na washindi watatu.
“Mshindi wa kwanza katika kila kanda atajishindia Shilingi Milioni 1, mshindi wa pili Shilingi laki 7, na mshindi wa tatu Shilingi laki 5, hivyo kufanya jumla ya zawadi za Shilingi milioni 15.4. Lengo la promosheni hii ni kuhamasisha wazazi kujenga utamaduni wa kuwawekea akiba watoto,” aliongezea Amina. Kushiriki katika promosheni hiyo, mzazi/ mlezi anatakiwa awe amefungulia akaunti ya “Junior Jumbo” mtoto wake na kumuwekea akiba mara kwa mara au kumfundisha kuweka akiba mwenyewe.
Mzazi anaweza kuweka fedha katika akaunti ya Junior Jumbo ya mtoto kwa kutembelea tawi, kwa CRDB Wakala, kwa kuhamisha fedha kutoka akaunti yake kupitia SimBanking au Internet banking au kutoka mitandao ya simu.
Kwa upande wake Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Buza, Mary Joshua alisema wazazi wengi wamekuwa wakipata changamoto katika kulipa ada za Watoto kutokana na wengi kutokuwa na utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya watoto. Hali hiyo imepelekea watoto wengi kuchelewa kurudi shule kuendelea na masomo au kujiunga na shule kwa wanafunzi wapya kutokana na kukosa mahitaji ya msingi ikiwamo ada.
“Tuna wahimiza wazazi/ walezi kuwafungulia watoto akaunti ya Junior Jumbo na kuanza kuweka akiba kwa ajili ya watoto kidogo kidogo. Akaunti hii inafunguliwa kwa vigezo nafuu sana, haina makato yoyote na hutoa faida ya riba kwa mteja,” amesema Bi. Mary Joshua huku akisisitiza kuwa Benki ya CRDB imejipanga kutoa elimu kwa wazazi ili kuwasaidia kuishi ndoto za watoto wao kwa kuwawezesha kupata elimu bora.
Meneja huyo alitoa rai pia kwa wazazi kutumia elimu inayotolewa na Benki ya CRDB kuwawekea akiba watoto wao kwani itasaidia sana kuweka msingi bora katika elimu. “Huu ni msimu wa sikukuu wengi wetu huwa tunafanya matumizi bila ya kujali January tunatakiwa kulipa ada pamoja na gharama nyengine za shule za watoto. Tunawahimiza kuweka akiba kwa ajili ya watoto kupitia akaunti ya Junior Jumbo,” aliongezea.