NA MWANDISHI WETU , GEITA
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo,Zitto Kabwe,amesema Chama hicho kinataka kabla ya mwisho wa mwaka huu Sheria ya mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011,ihuishwe kwa kuweka utaratibu mpya wa kukamilisha mchakato huo
Amesema sheria hiyo ianze kwa kuitishwa Mkutano wa Kitaifa kupata mwafaka wa masuala Maalumu kama vile muundo wa Muungano, kuundwa kwa timu ya Wataalamu ( committee of experts),itakayoandika Rasimu mpya ya Katiba na kura ya maoni ya Katiba Mpya.
Zitto alitoa kaauli hiyo leo Juni 4, 2022 mkoani Geita kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Nyankumbu na kueleza ni wakati muafaka sasa
Kutungwa kwa Sheria mpya ya Uchaguzi ili kuwa na hume huru ya Uchaguzi, Pamoja na Sheria mpya ya Vyama vya Siasa.
Amesema kwa sasa watanzania si watu wa kudai Katiba mpya bali wanapaswa kujielekeza juu ya wanaanzaje mchakato huo hadi katiba ikamilike
“Hivi sasa sio tunataka Katiba mpya au la, Suala hivi sasa ni tunaanzaje mchakato huo nimeeleza kuwa ACT Wazalendo inataka kabla ya mwisho wa mwaka huu yafuatayo yawe yamefanyika, kwanza sheria ya mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, ihuishwe kwa kuweka utaratibu mpya wa kukamilisha mchakato wa Katiba”
“Sheria hiyo ianze kwa kuitishwa Mkutano wa Kitaifa kupata mwafaka wa masuala Maalumu kama vile muundo wa Muungano, kuundwa kwa timu ya Wataalamu ( committee of experts),itakayoandika Rasimu mpya ya Katiba na kura ya maoni ya Katiba Mpya.”alisema Zitto
Ameongeza kuwa ni wakati wa kutoka kwenye maneno na kwenda kwenye vitendo kwa kuachana na mtindo wa kususa susa majadiliano yatakayozaa Katiba mpya na Tume huru ya Uchaguzi
“ Mabadiliko haya lazima yahusishe mabadiliko ya Katiba, wale wanaosema Katiba haileti chakula wanapotosha, Kwa kuwa bila ya kuwa na mfumo madhubuti wa kiuongozi unaosimamiwa na Katiba nzuri mambo hayo hayatafanyika” alisema na kuongeza
“Mfumo mzuri wa Katiba utaainisha Kila kitu kwa mfumo wake na hili linawezekana tukiwa na bunge linaloisimamia serikali”
Ametanabaisha kuwa kwa sasa mambo mengi hayaendi ipasavyo kwa kuwa Bunge limeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia serikali kwa kuwa lina wabunge wengi wa chama kimoja
Amesema kukiwa na Katiba nzuri watanzania watapata bunge zuri na kukiwa na bunge zuri litatekeleza wajibu wake wa kuisimamia serikali na ili ishughulike na shida za wananchi
“Tangu uhuru tunaongozwa na Chama cha Mapinduzi hatuwezi kupata mabadiliko ya kiuchumi, Machache yanayopatikana yangekuwa makubwa zaidi kama CCM ingekuwa nje ya utawala. Vyama vinapokaa muda mrefu kwenye uongozi vinaishiwa mawazo.”amesema
Akizungumzia sekta ya Mifugo kutowanufaisha moja kwa moja wakazi wa Mkoa wa Geita,Zitto Kabwe amesema Serikali inapaswa iwanue wafugaji ili ikuze uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa Ujumla.
Amesema ili kufikia hatua hiyo ni vema ikawatengea eneo kubwa wafugaji kwa ajili ya malisho na unywaji maji kwa mifugo pamoja na mazingira yatakayowawezesha kuwasomesha Watoto wao bila usumbufu wa kuhitaji kuhama hama
“Sekta hii ya Mifugo Ifungamanishwe na sekta ya Viwanda na Biashara kupitia TANTRADE tupate viwanda vya kutosha vya Maziwa,Nyama na mazao mengine kama Ngozi na Serikali ianzishe Bodi moja ishughulike na mazao yote ya Mifugo kuanzia nyama , maziwa, ngozi na kwato kwani sasa hivi kuna bodi ya maziwa tu”amesema Zitto Kabwe.
Ameeleza kuwa ni aibu kwa Tanzania ambayo ni nchi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya Ng’ombe katika bara la Afrika huku sekta hiyo ikichangia asilimia 7.0 kwenye pato la Taifa kwa mwaka 2022,licha ya kaya asilimia 35 kujishughulisha na masuala ya ufugaji
“Changamoto ya wafugaji Geita hususan katika maeneo ya Bukombe ni kutokuwa na maeneo ya maalisho ya mifugo, Mifugo inakamatwa Kwenye hifadhi (inaswagwa kwenda hifadhi inakamatwa Migogoro kati ya wakulima na wafugaji wanauana kwa kukosa maeneo hili suala linapaswa kutazamwa kwa kina na kulipatia ufumbuzi”amesema Zitto
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara Dorothy Semu amesema hali ya upatikanaji wa huduma za Afya kwa wakazi wa Geita ni ngumu kwa kuwa kila hatua inahitaji matumizi ya pesa ikiwemo kumuona daktari Pamoja na kupataa vipimo vya afya.
Amesema hali hiyo inatokana na serikali ya Chama cha Mapinduzi kugeuza afya ya Watanzania kuwa bidhaa badaala ya huduma
Kwa mujibu wa Sera ya Afya 2017 wazee,watoto chini ya miaka mitano na wajawazito huduma za Afya kwao ni bure hivyo tunawataka watumishi kuzingatia hili na kuwapa huduma kamili watu wa makundi haya na sio huduma nusunusu”amesema
Ameongeza kuwa ACT Wazalendo inaitaka Serikali ishiriki kuhudumia na kugharamia afya za watanzania kwa kutumia kodi zao badala ya kufanya kama bidhaa za sokoni.
“Suluhisho juu ya hali hii ni hifadhi ya jamii kwa wote Masikini wasiojiweza walipiwe na Serikali kwenye hifadhi ya jamii ili wapate Bima ya afya lakini pia mitaji ya kuanzisha shughuli za uzalishaji au biashara”amehitimisha