NA MWANDISHI WETU, IRINGA
BALOZI na Mwenyekiti wa Shina Namba saba la Chama cha Mpinduzi (CCM) katika kijiji cha Ilambilole wilayani Iringa ameangukiwa na bahati itakayomchukua maisha yake yote kuisahau baada ya msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo kupitisha mchango utakaowezesha kujengewa nyumba ya kisasa ya vyumba vitatu vya kulala.
Balozi Rose Nzelewela amekutana na bahati hiyo leo Mei 30, 2023 baada ya Mbunge wa Jimbo la Isimani William Lukuvi kuzungumzia wasifu na mchango wake kwa chama hicho ikiwa ni pamoja na vikao na mikutano yote ya shina hilo kufanyikia katika nyumba yake ya udongo aliyopanga.
Katibu wa Siasa, Itikiadi na Uenezi, Dk Sophia Mjema aliyeambatana na Chongolo katika ziara yao ya siku sita mkoani Iringa alikuja na wazo la kumjengea nyumba balozi huyo na kuanzisha harambee ya kuchangia ujenzi wake baada ya kupewa fursa ya kuwasalimia wanachama wa shina hilo lililopo katika kata ya Kising’a jimboni Isimani wilayani Iringa.
Akiahidi kuchangia tofali 2000, Dk Mjema alimuinua Mkuu wa Mkoa Halima Dendego aliyechangia mifuko 30 ya saruji huku Mkuu wa Wilaya ya Iringa naye akichangia mifuko 20.
Katibu Mkuu aliunga mkono harambee hiyo kwa kuchangia tofali za Sh.Milioni 1 huku Lukuvi akichangia Sh 400,000 kwa ajili ya kiwanja itakapojengwa nyumba hiyo.
Wengine waliochangia ni pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas atakayetoa mifuko 100 ya saruji na Sh.Milioni 2.5 zitakazogharamia ujenzi wa nyumba hiyo.
Naye Leonard Mahenda na Richard Kasesela ambao pia ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa walichangia mbao za kupaulia, misumari na mawe huku mjumbe wa kamati ya Utekelezaji ya UWT Taifa Fatma Rembo akichangia bati 100.
Wengine waliochangia ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Daudi Yasin aliyechangia milango na madirisha huku wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Iringa, Dickson Mwaipopo, Seki Kasuga, Zainabu Mwamwindi wakichangia kokoto, mawe, rangi na dali.
Shirika la Umeme Tanesco limeahidi kufunga umeme pindi nyumba hiyo itakapokamilika huku Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ikihadi kupeleka maji keshokutwa ili ujenzi uanze mara moja.
Akishukuru kwa msaada huo Nzelewela amesema ameupata kwa miujiza ya Mungu na kama Katibu Mkuu asingekutana na shina lake maisha yake yote yeye na familia yake yangeishia katika nyumba ya kupanga anayoishi hadi sasa.
“Niliamka kuandaa kikao hiki cha shina letu bila kujua kama kitanipa zawadi kubwa katika historia ya maisha yangu. Ningepata wapi fedha zote hizo kujenga nyumba ya kisasa?” alisema balozi huyo mwenye miaka 56.
Awali akimkaribisha Katibu Mkuu katika shina hilo, Lukuvi alimpongeza Chongolo akisema; “umeweka historia ndani ya chama hiki kwani haijawahi kutokea huko nyuma kwa kiongozi wa nafasi yako kushiriki kikao cha shina na kuwahutubia wanachama wake. Wewe ni Katibu Mkuu wa kwanza.”
Lukuvi alisema ziara za Chongolo kwenye mashina ya chama hicho itumiwe kupeleka ujumbe kwa viongozi wa ngazi zingine chini kote kuwa na utaratibu wa kukutana na wanachama katika vikao vyao vya mashina.
“Kama viongozi wa mikoa, wilaya na kata wakiiga utaratibu wako huu itaongeza uhai katika mashina yetu na itasaidia kuwafanya viongozi kuwa jirani na wanachama wao, kuwasikiliz na kuzipatia ufumbuzi changamoto zao,” alisema.
Katibu Mkuu aliwahakikishia wana CCM wa shina hilo kwamba chama chake kwa kupitia Mwenyekiti wake na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwamba ahadi zote zilizoahidiwa katika ilani yao zitatekelezwa, moja baada ya nyingine.
Chongolo alisema utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayojibu changamoto mbalimbali za wananchi inakifanya chama chao kuendelea kuwa imara na hivyo kuifanya nchi isiyumbe.
“CCM haitoi ahadi zake hewani. Tuliahidi kupitia Ilani yetu na kwa ridhaa yenu tumeweka mipango ya kutekeleza ahad…