NA DENIS CHAMBI, TANGA
MBUNGE wa jimbo la Tanga mjini ambaye pia ni waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema ujenzi na ukarabati wa masoko makubwa jijini Tanga utaanza muda wowote kuanzia sasa hivyo amewaomba wananchi na Wafanyabiashara kuondoa hofu kuwa masoko ya jiji hilo yamesahaulika.
Alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akihutubia wananchi wa kata ya Makorora kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama cha mapinduzi wilaya ya Tanga ambapo alisema kuwepo masoko hayo licha ya kuchangia pato katika halmashauri hiyo pia yamekuwa na tija kwa wananchi hao hasa wafanyabiashara wadogo wadogo.
“Wananchi hasa wafanyabiashara wadogo wadogo tunajua changamoto zilizopo hasa uchakavu na miunfombinu ya masoko , tupo kwenye mchakato wa ujenzi wa masoko ya kisasa yakiwemo masoko ya mlango wa chuma pamoja na hili la hapa Makorora hivyo niwaombe msiwe na hofu kabisa kuhusu masoko yetu ,soko letu la Makorora Sh.6 Bil.zimeshaletwa na hivi karibuni ujenzi utaanza rasmi na tutakuwa na soko la kisasa kabisa lakini pia tunayo masoko mengine ya Mgandini ambalo linahitaji zaidi ya Bil.16/- ili kukamilisha Ujenzi na Sasa hivi tunatafuta wadau lakini soko la mlango wa chuma pesa ipo tayari zaidi ya Mil.200 /-na ukarabatI utaanza Wakati wowote na hii itawasaidia wafanyabiashara na wananchi kupata huduma kwa urahisi zaidi “alisisitiza Ummy
Wakati huo huo Waziri Ummy aliwatoa hofu wanufaika mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri nchini kwaajili ya vijana, akinamama na watu wenye ulemavu kuwa serikali ipo kwenye marekebisho ya njia bora zaidi za upataji wa mikopo ya halmashauri kwa urahisi ilkiwa pia ni mkakati wa kukwepa na kuwabana wanapotumia fedha hizo kinyume na malengo ya serikali.
“Naomba niwatoe hofu juu ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri,msihofu mwezi wa 7 itaanza kutolewa kwa utaratibu mzuri zaidi ya awali serikali ipo inawawekea wanufaika wote mazingira rafiki ya kuweza kupata mikopo hii na kuweza kuondokana na mikopo umiza ambayo mmekuwa mkipewa ” alisema waziri Ummy
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga Abdulrahman Shillow aliwataka wananchi kupuuzia taarifa zilizotolewa hivi karibuni na Viongozi wa vyama vya siasa Jijini Tanga kuwa halmashauri hiyo imetafuna fedha za ununuzi wa magari kwa shughuli mbalimbali ikiwemo yakuzolea takataka.
“Hivi karibuni Kuna wanasiasa walitoa Taarifa za kupotosha kwenye majukwaa kuwa Halmashauri yetu Kuna Watumishi wametafuna hela za magari ya Taka, naomba niwaambie magari yapo na mwenge utazindua”alisema Shillow
Kauli hiyo imekuja kufwatia hoja za viongozi wa chama cha ACT Wazalendo ambao walifanya mkutano wao wa hadhara hivi karibuni katika kata ya Ngamiani kati ambapo walihoji uwepo wa upigaji wa fedha za halmashauri hiyo ambazo hazijulikani zilikokwenda wala matumizi yake.
Awali akizungumza katibu wa chama hicho wilaya ya Tanga Selemani Sankwa amewataka wananchi kuwapuuza na kutokuyumbushwa na baadhi ya wanasiasa wanao tangaza nia za kutaka kugombania nafasi mbalimbali ndani na nje ya chama akiwaonya kuwa hoja zao kwa sasa hazina mashiko badala yake wawaache viongozi wafanya kazi.