NA MWANDISHI WETU, IRINGA
MRADI wa bwawa la kuhifadhi maji uliojengwa katika kata ya Masaka wilayani Iringa kwa Sh.Bilioni 1.5 umeibua mradi wa ufugaji wa samaki uliozinduliwa leo Meo 29, 2023 na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo.
Chongolo amezindua mradi huo kwa kupandikiza vifaranga vya samaki 3,000 kwenye bwawa hilo huku yeye mwenyewe akichangia Sh milioni moja zitakazonunua vifaranga vingine 8,000.
Mchango wa Chongolo uliungwa mkono na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Leonard Mahenda na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa Dickson Mwaipopo ambao nao walichangia kiasi kama hicho na hivyo kufanya vifaranga vya samaki vitakavyopatikana kwa fedha hizo kuwa 24,000.
Pamoja na mradi huo wa samaki, Diwani wa Kata ya Masaka Mathew Nganyagwa alitaja manufaa mengine yatakayotokana na bwawa hilo kuwa ni pamoja kuwezesha kilimo cha umwagiliaji, uanzishwaji mradi wa maji safi na salama kwa matumizi ya wananchi na kujenga mabirika kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
Akipanda vifaranga hivyo 3000 katika bwawa hilo Katibu Mkuu wa CCM aliwataka wananchi wa kata hiyo kujiongeza zaidi kwa kufikiria kuanzisha mashamba ya vyakula vya mifugo kwa kuwa mahitaji yake katika soko yanazidi kuongezeka.
“Aidha mnaweza pembezoni mwa bwawa hilo kupanda vitindi vingi kwa ajili ya kuzalisha ulanzi ili kuenzi mila za wahehe,” alisema.
Aliwataka wananchi wa kata hiyo kuacha kuwasikiliza watu wenye dhamira inayolenga kukwamisha au kuzorotesha maendeleo ya watanzania akisema CCM chini ya mwenyekiti wake Rais Dk Samia Suluhu Hassan itatekeleza ahadi zake zote ilizoahidi kupitia Ilani yake ya uchaguzi.
Akitoa taarifa ya ufugaji samaki katika halmashauri hiyo, Ofisa Uvuvi Kelvin Ndege alisema wameendelea kuwahamasisha wananchi juu ya ufugaji wa samaki wakitambue mchango wake kilishe na kiuchumi.
“Kwa mwaka 2022/2023 wananchi katika halmashauri hii ya wilaya ya Iringa wamehamasika kuchimba mabwawa 109 na kuanza kufuga samaki,” alisema na kuongeza kwamba halmashauri hiyo mpaka sasa ina jumla ya mabwawa 350.
Akizungumzia bwawa hilo la Masaka lenye uwezo wa kupandwa samaki 1,318,172 alisema limejengwa kwa usimamizi wa Wizara ya Maji chini Bodi ya Maji Bonde la Rufiji.
Alisema bwawa hilo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 5.33 sawa na ekari 533 lina uwezo wa kuhifadhi maji zaidi ya mita za ujazo 439,803 zitakazohudumia zaidi ya wananchi 10,000 ndani na nje ya kata hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga alizungumzia manufaa ya bwawa hilo kuwa ni pamoja na kuboresha lishe na kuondoa udumavu katika kaya, na kuongeza kipato cha jamii na ajira kwa vijana wanaojishughulisha na uvuvi, usafirishaji wa biashara kwenye mnyololo wa samaki.