NA TATU MOHAMED
ZAIDI ya wajawazito 2000 wilayani Korogwe mkoani Tanga wameshiriki katika mbio za Mamathon ambazo zimefanyika kwa mara ya kwanza wilayani humo.
Mbio hizo ambazo zimefanyika jana zimeandaliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Jokate Mwegelo lengo lake ni kutoa hamasa kwa wajawazito kujifungua salama na kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Akizungumza na wananchi wa Korogwe mara baada ya kumalizika mbio hizo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) Mary Chatanda amewataka wahudumu katika vituo vya afya, Zahanati na Hospitali zote kuzingatia maadili ya kazi zao na kuepuka na vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya kazi.
“Hivi karibuni tumesikia tukio lililotokea wilayani Kaliua mkoani Tabora la kuuliwa na kuchukuliwa viungo vya watoto wachanga. Ni tukio baya, tunalikemea na tunaiomba serikali iendelee kuchukua hatua kali kwa watumishi wasio na maadili kama hawa na waendelee kutoa mafunzo na kuwakumbusha wajibu wao.
“Nitoe wito kwa watumishi wa afya wote acheni kujihusisha na vitendo visivyo na maadili, tunafahamu kazi yenu ni wito hivyo mtende haki. Muwe na lugha nzuri kwa wagonjwa, mimi sitakubali kuona mjamzito ananyanyaswa muwahudumie kwa huruma,” amesema Chatanda.
Aidha ametoa wito kwa wajawazito kuacha tabia ya kujifungulia majumbani na badala yake wawahi katika vituo vya afya.
“Mnapopata dalili za kujifungua wahini katika vituo vya afya mpate huduma bora ambayo itamsaidia mama na mtoto kuwa salama,” amesisitiza.
Pia amewataka wananchi wa Korogwe kumtumia Mkuu wa Wilaya huyo kwani ana mambo mazuri yatakayowezesha kuwaletea maendeleo na wao kama viongozi wa Chama na Serikali watatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha anatekeleza majukumu yake vizuri.
“Tunakupongeza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na kote alikopita amekuwa akifanya kazi nzuri hivyo wananchi wa Wilaya ya Korogwe wajue wamepata jembe na ndio maana Rais Dkt Samia Hassan Suluhu ameendeea kumteua katika nafasi hiyo ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe .
“Wananchi wa Korogwe mmepata jembe na muendelee kumpa ushirikiano na sisi viongozi tutaendelea kumuunga mkono na katika hili la ambalo ameliazisha aendelee nalo kwani linagusa maisha ya wamama wajawazito na watoto moja kwa moja kulinda afya zao, ” amesema Chatanda.
Awali akizungumza na wananchi hao, Jokate amesema lengo la kufanya tukio hilo ni kuenzi yale yote ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameyafanya kwaajili ya kusaidia wanawake na watoto.
Amewapongeza wajawazito pamoja na wote walioshiriki na kumaliza mbio hizo kwani kufanya mazoezi kwa mjazito kuna faida nyingi.
Amewataka kuhakikisha baada ya mbio hizo wanaendelea kushiriki mazoezi, kuzingatia lishe bora kipindi chote cha ujauzito wao jambo litakalosaidia kujifungua salama na kuwezesha mpango wa Serikali wa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.