NA MWANDISHI WETU, LINDI
SOMOE Saidi (65) mkazi wa Kijiji cha Nachiu, Kata ya Nyengedi Halmashauri ya Mtama, mkoani hapa amefariki dunia kwa kuliwa na mamba alipoenda kuoga katika Mto Lukuledi.
Taarifa kutoka kwa watu wa karibu na marehemu wanaeleza kuwa, siku ya tukio mama huyo alienda mtoni kwa ajili ya kuoga na kuchota maji, lakini baada ya muda kupita wanakijiji wengine walienda mtoni ndipo wakakuta ndoo ya maji pamoja na nguo pembezoni mwa mto huo.
“ Bila kutambua zile nguo na ile ndoo ni ya nani ila walianza kutilia mashaka kuwa huenda aliekuwepo eneo lile amechukuliwa na mamba, kwani tofauti na vitu hivyo vilivyokutwa, pia kulikuwa na damu pamoja,” anasema mmoja kati ya ndugu hao.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Alhaji Salim Kabeleke amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Mei 24, 2023 na kwamba mwili ulipatikana siku tatu baadaye, baada ya kufanya msako kwa kushirikiana na askari wa maliasili, lakini baadhi ya viungo vilikuwa vimeliwa.
Amewataka wakazi wanaoishi na kufanya shughuli zao karibu na Mto Lukuledi kuwa makini na mamba, huku akiwaomba kushirikiana na watu wa maliasili, ili kutambua maeneo hatarishi ya makazi ya mamba hao.