NA TATU MOHAMED, KOROGWE
KATIKA kuhakikisha maisha ya mjamzito na anayenyonyesha yanakuwa salama, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Joketi Mwegelo, amezindua mbio za wajawazito zitakazofanyika Mei 28 mwaka huu.
Mbio hizo zenye jina la Mamathon zitakuwa na kauli mbiu ya Mwendo wa Mama.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbio hizo uliofanyika katika Wilaya hiyo mkoani Tanga, Mwegelo amesema mbio hizo zitaanzia ofisini kwake kuelekea viwanja vya shule ya msingi ya Mazoezi.
Amesema Mamathon itakuwa ni ya aina yake kufanyika na lengo lao ni kuwahamasisha wakina mama na kuondoa dhana potofu wanazozipata pindi wanapokuwa na ujauzito.
“Nadhani wengi hamjawahi kuona wanawake wajawazito wakikimbia sasa mtawaona Mei 28 mwaka huu tuna jambo letu mapema,” amesema.
Amesema kwa kutambua mwendo wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo wameona kama viongozi kuwa na wajibu wa kuwakutanisha jamii na kuyaenzi yale serikali yanayofanya.
“Hii kauli mbiu yetu ya Mwendo wa Mama ni kutambua mchango wa Rais Samia jinsi anavyoitumikia Tanzania hususani alivyoigusa kundi la akina mama kwenye kila pembe na kila kona ya nchi,” amesema Jokate.
Aidha, amesema katika mbio hizo watatoa elimu ya afya ya uzazi na lishe lengo ikiwa ni kuhakikisha mama na mtoto wanakuwa afya njema.
“Hiyo siku tutazindua lishe bora ili tunapokuwa na lishe bora vizazi vyetu vinavyozaliwa vitakuwa na lishe nzuri na akili timamu na kujenga uchumi wa nchi hii pia ni ajenda ya Rais Samia,”amesema.
Mwegelo amesema mbio hizo pia zinawahusu wanawake wote, hivyo ni muhimu kujiandikisha katika vituo vya afya na hospitali ili takwimu kamili ipatikane na wale wajawazito watapatiwa zawadi kwa ajili ya kuwasaidia kujifungua salama.
Amesema ili kuandaa zawadi hizo ni lazima wapate idadi ya wanawake hao kwa ajili ya maandalizi ya siku hiyo muhimu.
Aidha, amewataka wananchi wa Korogwe kuacha mtindo wa kutupa watoto na badala yake wajitahidi kutimiza wajibu wao wa kuwalea.
Amesema hivi karibuni wameokota kitoto kichanga na kufanikiwa kuokoa maisha yake na kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kupatiwa huduma katika kituo cha afya.
Naye, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Korogwe, Salma Swedi, amesema wanamshukuru Rais Samia amewafanyia mambo makubwa hasa katika sekta ya afya wameweza kupokea Sh. Bilioni 1.6 ambazo zimeelekezwa katika miundombinu mbalimbali ikiwemo jengo la dharura.
Amesema jengo hilo limegharimu Sh. milioni 300 na limesaidia kuokoa dhararu ambazo zinatokea barabarani ikiwemo ajali zinazotokea.
“Ujio wa jengo hilo limesaidia kupunguza adha kubwa kwa wagonjwa na kuokoa maisha ya wagonjwa. Pia tumeongezewa vituo vya afya viwili awali tulikuwa na kituo kimoja hivi sasa tuna vituo vitatu katika Halmashauri hii,” amesema.