NA MWANDISHI WETU, TABORA
WATOTO mapacha waliozaliwa kabla ya muda (njiti) katika Kituo cha Afya Kaliua mkoani hapa na baadaye kupoteza maisha wanatarajiwa kuzikwa leo. Watoto hao mmoja wao alikutwa ameondolewa ngozi kwenye paji la uso na kuharibika jicho moja la upande wa kulia.
Baba mzazi wa watoto hao, Isaka Rafael (27) amekubali kupokea miili ya watoto hao kwa ajili ya maziko.
Rafael alitoa uamuzi huo jana alipozungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu akiwa wilayani Kaliua mkoani hapa na akasema yupo tayari kuzika wanawe.
Alisema ameamua hivyo baada ya kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Mkoa wa Tabora. Rafael alisema watoto hao watazikwa leo nyumbani kwao katika Kata ya Muungano, Kijiji cha Kalemela (B), Kitongoji cha Mwangaza Wilaya ya Kaliua mkoani humo.
Alisema kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dk Batilda Burian imeifariji familia yake na wanaamini kwamba waliohusika katika vifo vya watoto hao wanachukuliwa hatua. Rafael aliishukuru serikali kupitia Wizara ya Afya, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kaliua na wadau wa ushirikiano wao.
Mei 22 , 2023 Dk Burian alisema watumishi wanne wa kituo cha afya Kaliua wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wajibu mashitaka ya kuhusika na vifo vya watoto hao katika mazingira ya utata.
Alisema uchunguzi kuhusu vifo vya watoto hao waliozaliwa njiti Mei 9, mwaka huu saa 5 usiku kituoni hapo umekamilika. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi alithibitisha kukamilika kwa uchunguzi wa tukio hilo na jalada linatarajiwa kufikishwa leo kwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali kwa ajili ya hatua za kisheria.
“Mahojiano ya tukio hili limefanyika kwa umakini mkubwa na watu wengi tayari wamehojiwa juu ya jambo hilo hivyo watu mbalimbali kwa kipindi hiki wanapaswa kutulia wakati serikali ikilishughulikia sakata hili,” amesema Kamanda Mbogambi.