DENIS CHAMBI, TANGA
CHAMA cha ACT Wazalendo mkoani Tanga kimesema kuwa changamoto zinazowakumba wafanyabiashara hapa nchini zisimalizwe kisiasa.
ACT wametaka itafutiwe mbinu mbadala wa kuondoa vikwazo wanavyokabiliana navyo ikiwemo kuundwa kwa tume maalum itakayotoa bei elekezi ili kuondokana na adha mbalimbali zinazoweza kujitokeza.
Wakisisitiza kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika soko la Ngamiani ,Thobias Haule ambaye ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Tanga na mjumbe wa ngazi za juu na ni Diwani wa Kata ya Mayomboni wilayani Mkinga Musa Jangwa wamesema kuwa zipo changamoto nyingi zinazowakumba wafanyabiashara ambazo zisipopatiwa ufumbuzi wa haraka zinaweza kupelekea mfumuko wa bei ukazidi kuwaumiza wananchi wa hali ya chini .
Haule amesema kuwa kuna hoja mbalimbali juu ya madhila yanayowakumba wafanyabiashara hapa nchini huku changamoto zikionekana kufanana zinapaswa zitatuliwe haraka ili kurahisisha wananchi kupata bidhaa kwa gharama nafuu na kupunguza mfumuko wa bei za bidhaa ukiwemo za chakula .
“Changamoto zinajulikana na zipo kwenye mfumo , changamoto za wafanyabiashara zinalingana kila sehemu , wananchi tuamke tudai haki zetu ,tusipo amka kusimamia haki zetu hakuna atakayetusaidia ” amesisitiza Haule
Kauli hiyo imekuja kufuatia mgomo wa wafanyabiashara ulioibuka hivi karibuni jijini Dar es salaam katika soko la kimataifa la Kariakoo ambapo mara baada ya Waziri mkuu Kassim Majaliwa kuzungumza na wafanyabiashara hao aliunda Tume Maalum itakayopitia changamoto mbalimbali zinazowakabili ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Haule amesema bado zipo changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara hasa wa hali ya chini ikiwemo mazingira duni licha ya kuwajibika kulipa kodi hali ambayo inayosababisha mzoroto wa kiuchumi huku ubambikizaji wa kesi kwa wananchi ukiwa nao ni kero akiiomba serikali kuzitazama kwa ukaribu.
“Kuna ubambikizaji mkubwa wa kesi hii nayo iangaliwe upya na ifanyiwe kazi haraka , wananchi wanahitaji huduma bora ya maisha ikiwamo bidhaa za vyakula kuwa chini wengi wa wafanyabiashara wakiwemo wamachinga wanafanya shughuli zao katika mazingira magumu na yanawanyima haki yao wakati huo huo wakiwa wanalipa kodi tunaitaka serikali iwatazame sana wafanyabiashara hawa na kuwawekea mazingira mazuri. ” amesisitiza Haule
Aidha alihoji mkoa wa Tanga kufungwa viwanda huku baadhi vikihamisha mitambo kupelekwa nje ya mkoa huo hali ambayo inazidi kuchangia kushuka kiuchumi na kuikosesha serikali mapato.,
“Tanga ilikuwa ni kimbilio la ajira nchini ,kila mmoja alikuwa anakimbilia Tanga kupata ajira katika viwanda mbalimbali vilivyokuwepo wakati ule lakini leo hii yamebakia magofu tu ,tunaomba waliopo kwenye madaraka watuambie na watuletee majibu ya maswali ya wakazi wa Tanga kuhusu viwanda” amehoji Haule