NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanasimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ukusanyaji wa mapato ili kuweza kufikia malengo yaliyopangwa.
Kairuki ameyasema hayo leo Mei 23, 2023 katika kikao kazi cha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ambapo wamejadili utekelezaji wa hoja za ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Amesema kuwa mwaka wa fedha 2022/2023 unatarajia kuisha ifikapo Juni 30, 2023 hivyo ni wajibu wa wakuu wa mikoa kuhakikisha wanasimamia kwa karibu ukusanyaji wa mapato kwenye halmashauri zao.
Kairuki pia amewataka wakuu wa mikoa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ili fedha zinazotolewa ziendane na thamani ya fedha inayotolewa na Serikali.
Pia amewataka kuzisimamia na kuhakikisha halmashauri zinajibu hoja za ukaguzi zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na maagizo ya Kamati za Kudumu Za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC).
Vile vile ameelekeza kushughulikia kero za wananchi ili kupunguza malalamiko pamoja na kujua hoja zilizotolewa kama zimeweza kutatuliwa kwa wakati.