NA MWANDISHI WETU
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, leo Jumapili, Mei 21 amemaliza ziara ya mikutano mkoani Kigoma.
Lissu pamoja na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakiongoza timu mbili tofauti, walikuwa wanazunguka kwenye majimbo yote ya mkoa wa Kigoma wakifanya mikutano ya Operesheni iliyozinduliwa na chama chao waliyoiita jina la +255.
Lissu alihitimisha mkutano wake wa mwisho kwenye kata ya Nguruka iliyopo jimbo la Kigoma Kusini leo jioni na msafara wake utakwenda mkoa wa Katavi ambapo operesheni hiyo itahamia huko.

Kwa upande wake, Mbowe atahitimisha ziara yake mkoa wa Kigoma kesho Jumatatu ambapo anatarajia kufanya mikutano kwenye majimbo ya Kigoma Kaskazini na Kigoma Kusini kabla ya kuelekea Katavi kuungana na makamu wake.
