NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WATUMISHI wa Umma 2060 wamefikishwa mahakamani kati ya mwaka 2010 hadi 2020 wakishtakiwa kwa makosa ya rushwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 ya Sheria za Tanzania.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Jakaya Kikwete wakati akijibu swali la Dennis Londo, Mbunge wa Mikumi aliyetaka kujua watumishi wangapi wa umma wamefikishwa mahakamani kwa rushwa na walioshinda kesi na kurejeshwa kazini kwa kipindi cha 2010 – 2020.
Akijibu swali hilo Bungeni Jijini Dodoma leo Mei 19, 2023, kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo, Kikwete amesema kati ya watumishi hao walioshtakiwa, watumishi 1,157 walitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu mbalimbali kwa mujibu wa sheria, huku watumishi 863 wakishinda kesi na kuachiwa huru kuendelea na kazi.