NA MWANDISHI MAALUM, MANYARA
WAGONJWA 11, 000 wenye tatizo la shinikizo la juu la damu hupata matibabu ya ugonjwa huo kila mwaka katika vituo vya afya vilivyopo Mkoa wa Manyara.
Hayo yamesemwa na mgeni rasmi wa maadhimisho ya siku ya Shinikizo la juu la damu Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara Dk.Yesige Mutajwaa wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika Kitaifa leo Mkoani Manyara.
Dk.Yesige ambaye pia daktari bingwa wa magonjwa ya ndani alisema idadi hiyo sio idadi kamili ya watu wenye shinikizo la juu la damu kwani hao elfu 11 ni idadi ya wale tu wanaopata matibabu katika Mkoa huo.
“Tangu mwaka 2018 hadi 2022 mwelekeo wa shinikizo la juu la damu kwa wananchi wa Manyara unaonyesha kuongezeka, mwaka 2018 wananchi wote walioudhuria vituo vya kutolea huduma za afya asilimia 0.9 walikutwa na shinikizo la juu la damu ambalo kila mwaka limekuwa likiongezeka hivyo mwaka 2022 wagonjwa wa shikikizo la juu la damu walioudhuria vituo vya afya Manyara kufikia asilimia 1.4”, alisema Dk.Yesige
Dk. Yesige alisema kumekuwa na changamoto ya uhaba wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya, lakini wao kama Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara wamejipanga na kuwapa uwezo wataalam weo kuweza kufanya maoteo vizuri ya dawa ili wananchi wanapofika katika Hospitali hiyo wasikutane na changamoto dawa.
Aidha Dk.Yesige ameishukuru Wizara ya Afya kwa kukubali na kuuchagua mkoa wa Manyara kuwa sehemu ya maadhimisho ya siku ya shinikizo la juu la damu kitaifa kwani kupitia maadhimisho hayo kunatoa hamasa kwa wananchi wa Manyara kuona umuhimu wa kupima shinikizo la juu la damu mara kwa mara.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo alisema JKCI ilianzisha kambi maalum za matibabu ya moyo lengo likiwa kusogeza huduma karibu na wananchi, kujengeana uwezo watumishi wa afya, pamoja na kuielimisha jamii juu ya magonjwa yasiyoambukiza.
Dk Pallangyo alisema magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu yameongezeka katika jamii hivyo ni wakati muafaka kama wadau wa afya kupigia kelele kuipa hamasa jamii kuhusu uelewa wa magonjwa hayo ili kwa pamoja jamii iweze kujikinga.
“Hadi sasa JKCI imeshatoa huduma na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza katika mikoa 10 ikiwemo mkoa wa Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Zanzibar, Iringa, Dodoma, Dar es Salaam, Pwani, na Manyara”,
“Kupitia kambi maalum za matibabu ya moyo tulizoziendesha tumeshatoa huduma za upimaji wa shinikizo la juu la damu pamoja na moyo kwa watu zaidi ya elfu 8 ambapo katika maeneo yote tuliyopita ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ndio ulioongoza katika magonjwa yote ambayo tumeweza kuyatambua”, alisema
Kwa upande wa huduma zinazotolewa JKCI Dk.Pallangyo alisema kila wagonjwa 7 kati ya 10 wanaofika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ajili ya huduma tatizo wanalokutwa nalo ni shinikizo la juu la damu, na matokeo hayo pia huonekana katika jamii kwani katika kambi wanazozifanya kati ya wagonjwa 4 kati ya 10 hukutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.
Naye Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukiza Wizara ya Afya Anzibert Rugakingira alisema Wizara ya afya yenye jukumu la kulinda afya za wanzania ipo mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanajua namba zao za shinikizo la juu la damu kujitambua na kupatiwa matibabu mapema.
Dk.Rugakingira alisema ni muhimu kila mtu akawa na utaratibu ya kupia shinikizo la juu la damu angalau mara mbili kwa mwaka ili pale mtu anapokuwa na tatizo hilo aweze kupata matibabu kwa haraka kupunguza athari anazoweza kupata kama hatatibiwa mapema.
Dk.Rugakingira alisema Wizara ya Afya inao mpango wa taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, mpango huo ulianzishwa baada ya kuwepo na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza hapa nchini.
“Kwa muda wa kipindi cha miaka mitano utafiti umefanyika ambapo 2017 wagonjwa wa shinikizo la juu la damu walioudhuria vituo vya afya walikuwa 688,000 mwaka 2022 wagonjwa hao waliongezeka hadi kufikia 1, 4000, 000 wagonjwa hawa ni wale tu wanaoudhuria kliniki naamini wapo wagonjwa wengi ambao hupoteza maisha yao bila ya kufika Hospitali kupata huduma” alisema Dk.Rugakingira