NA MWANDISHI WETU, TABORA
SERIKALI imewasimamisha kazi baadhi ya watumishi wa afya katika Kituo cha Afya cha Kaliua na kumuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) kusimamia weledi, maadili na miiko ya watumishi wa afya baada ya raia mmoja kulalamika juu ya huduma zilizotolewa na kupelekea watoto wake mapacha ‘kuuawa’.
Jeshi la Polisi ambalo pia limetajwa katika walaka uliochapishwa na msamaria mwema Malisa J. likinukuu maelezo ya Kisaka Mtoisenga ambaye ni Mkazi wa Ushikola wilayani Kaliua mkoani Tabora, halijatoa tamko rasmi.
Katika andiko lake, Mtoisenga amesema alimpeleka mkewe katika kituo hicho akiwa na ujauzito wa miezi saba. Wauguzi walimpatia huduma na kujifungua watoto njiti hata hivyo kutokana na Kituo hicho kutokua na uwezo wa kuwahudumia watoto hao kilitoa rufaa.
Hata hivyo wazazi hao ambao walikoswa gari la wagonjwa iliwabidi wakodi bajaj. Wakati wauguzi wakidai walikuwa wakiwaandaa watoto hao kwa ajili ya safari, iliwachukua saa kadhaa kabla ya kuwakabidhi wakiwa kwenye boksi huku wakionekana kunyofolewa macho, ulimi na kuchunwa ngozi.
“Tulipofika nje kabla ya kupanda gari tukafungua mabox. Tukakuta watoto wameng’olewa macho, wamekatwa ulimi na wamechunwa ngozi kwenye paji la uso. Tukahamaki. Tukarudi kuuliza nini kimetokea, hawakutupa majibu ya kuridhisha.
“Tukaenda Polisi, lakini wakatuambia tukazike tu maana wao hawashughuliki na ushirikina. Tukaenda kwa Mkuu wa wilaya, alipoona maiti akasema huo ni Ushirikina. Akatushauri tukazike tu maana hata tukienda mahakamani hatuwezi kushinda. Nikamuuliza kwanini ushirikina ufanyike hospitalini? Nikakataa kuzika.
Nikataka uchunguzi ufanyike. DC akaagiza maiti zipelekwe hospitali ya Urambo. Hadi leo zipo huko sijui nini kinaendelea. Naomba unipazie sauti Rais asikie. Watoto wangu wametendewa unyama kwenye kituo cha afya, halafu nanyimwa haki kwa kisingizio cha ushirikina? Naumia sana,” ameandika Kisaka.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema serikali imefuatilia tuhuma hizo na kusema “kuna ukweli.”
“Uongozi wa Wilaya Kaliua umeshaanza kuchukua hatua. Baadhi ya Watumishi wa Afya waliomuhudumia mama huyu wameshasimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kwa kuwa Usiku wa tukio wodini kulikuwa na watumishi, wagonjwa na ndugu wa wagonjwa ambao walikuwa wakiangalia wagonjwa wao.
Mwanafunzi wa Shahada ya Udaktari, Emmanuel Mathias amehoji iweje kituo cha afya kiliruhusu kumpokea na kumhudumia mama mwenye ujauzito wa miezi saba wakati wakijua hawana vifaa na iweje walikaa na watoto kwa saa zote wakati wakijua ni watoto njiti.
Serikali imesema itatoa ufafanuzi wa kina kuhusu jambo hili.