NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa wafanyabiashara Karikaoo, Martin Mbwana amesema mgomo unaoendelea sasa unatokana na ushawishi wa kikundi cha watu wachache wenye maslahi yao binafsi na kuomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi yake.
Akizungumza leo Mei 16, 2023 amesema mgomo unaoendelea unasababishwa na kikundi cha watu wachache wenye maslahi yao binafsi.
Amesema, jana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (sasa amehamishiwa Mkoa wa Mwanza), Amos Makalla alifika na kuwasihi wafungue biashara, lakini waligoma na kusema wanataka kuonana na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Bahati nzuri mama ni msikivu, Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) akaja tukawa nae kwenye kikao chake cha ndani kuanzia saa nne mpaka saa sita, baadae tukamuomba Waziri Mkuu aende Kariakoo akaongee na wafanyabiashara, Waziri Mkuu alienda na akawambia ameagizwa na Rais na akawaomba na kuwasihi wafungue biashara, anakwenda msibani leo, kesho tarehe 17 atakuja na atawaagiza mawaziri husika na wabunge wa Mkoa huu, waache bunge waje Dar es Salaam tukutane nae tuzungumze.
“Shida ni kikundi cha watu wajanja ndio maana nimeomba vyombo vya usalama vifanye kazi yake, jumuiya hizi kuna ambao wananufaika na migogoro ndio maana wanaichochea kwa manufaa yao.
“Inachochea watu ionekane serikali ya mama Samia haisikilizi watu au Waziri Mkuu hajaja kuongea na wafanyabishara, ni baadhi ya watu, kuna watu wanapita chini chini wanashawishi wafanyabiashara wafunge maduka, Rais kashamtuma mtendaji wake aje unafunga maduka ili aje nani?
“Nimeagiza na nimewaomba vyombo vya usalama vifanye kazi yake. Wakitaka ushirikiano kwangu nitatoa asilimia 100 wao ndio wanajua wafanyeje,” alisisitiza Mbwana.
Maduka mengi yaliyofungwa, ni yale yanayouza nguo, viatu, vyombo, vitenge, mapazia huku yaliyofunguliwa yakiwa ni yale ya vifaa vya matairi, vioo, urembo vyombo vya ndani na maduka ya vitambaa vya nguo.
Hata hivyo maduka mengi yaliyowazi, ni yale yaliyopo pembezoni mwa soko huku asilimia kubwa ya maduka ya katikati yakiwa yamefungwa.
Miongoni mwa kero zilizokuwa zikilalamikiwa na wafanyabiashara hao, ni kamatakamata ya wafanyabiashara, utoaji wa risiti za kielektroniki na kudai kuwa unaua biashara. Wafanyabiashara hao pia wanalalamikia sheria mpya ya usajili wa stoo.