NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda ,amesema kazi ya kukusanya maoni ya kuboresha mitaala na sera ya elimu inaendelea, watachakata maoni yote ili kupata kitu kizuri chenye tija kwa taifa.
Prof. Mkenda ameyasema hayo leo Mei 14, 2023 Jijini Dodoma wakati wa kufunga Kongamano la kujadili sera na mitaala mipya ya elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu lililofanyika siku tatu.
Amesema kuwa nia ya Serikali ni kufanya maboresho makubwa kwenye sekta ya elimu hivyo kamati haitaacha maoni yoyote ambayo yanatija katika kuboresha mfumo wetu wa elimu nchini.
“Niwahakikishie hakuna maoni yatakayoachwa yote tutazingatia na tutayabeba kwa ajili ya utekelezaji nashukuru kuna baadhi ya maoni yametolewa ufafanuzi hapahapa”amesema Prof.Mkenda
Aidha amesema Wizara itazingatia maoni yaliyotolewa na wadau kwenye kongamano hilo na malengo yaliyopo ukusanyaji maoni utaendelea hadi Mei 31, 2023.
“Tumejiwekea malengo ifikapo Mei 31, tuwe tayari kusonga mbele, tulikuwa tunasikiliza kwa makini sana maoni nimeona hakuna upinzani katika mambo muhimu ya mageuzi ya sera.”
“Kuna maoni elimu ya awali iwe ya lazima ni suala ambalo hata kamati ya bunge walisisitiza na sisi tumesema tunalipokea tunalichakata na kuliangalia, hatuwezi kusema kwa haraka kwamba litakuwa lazima lazima tuangalie uwezekano wa utekelezaji,”amesema Prof.Mkenda
Hata hivyo amesema baadhi wameshauri elimu ya lazima iwe miaka 11 ambayo inajumuisha elimu ya awali nayo iwe lazima na sera ya mwaka 2014 ilikuwa inataka elimu ya lazima iwe miaka 10 lakini utekelezaji ulikuwa miaka 7 na kubainisha kuwa watalichakata jambo hilo kwa umakini mkubwa.
Waziri Mkenda amesema kwenye mapitio ya sera yamegusa hadi vyuo vikuu na suala la mitaala litaendelea kuwa endelevu.
“NACTVET wanakamilisha utafiti waliofanya kwa waliohitimu vyuo vya ufundi vya VETA wapo wapi na wanafanya nini, na kuchunguza kwenye magereji, hoteli wameajiri wangapi kutoka VETA.”
Ameongeza kuwa “tunataka tutengeneze elimu ya kiujitegemea na tutengeneze uwepo wa wahitimu wenye uelewa na wenye jeuri ya kuhoji na katika bajeti tumetenga tayari kuwaandaa walimu kuendana na mabadiliko hayo tija ipatikane” amesema.
Hata hivyo amesema kuwa watahakikishie katika mafunzo ya amali hasa tunataka tusiyafanye watu wakayadharau na ndio maana hasa ya kuanza na vyuo vya ufundi, mafunzo ya amali sio ya waliofeli bali waliofaulu vizuri.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Deogratius Ndejembi,amesema kama TAMISEMI haitakuwa kikwazo katika kutekeleza sera mpya ya elimu itakayopitishwa.
Ameongeza kuwa “mpaka sasa tuna shule 9 za ufundi na kupitia mradi wa SEQUIP tuna kiasi cha bilioni 300 tuna kwenda kujenga shule za ufundi katika karibu Halmashauri zote ambazo hazikufikiwa na vyuo vya VETA tunakwenda kujenga madarasa hayo” amesema Ndejembi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu,Utamaduni na Michezo Prof.Kitila Mkumbo,amesema wao kama wawakilishi wa wananchi Bungeni watahakikisha wanasimamia maoni yote ya wadau yanafanyiwa kazi kikamilifu ili tija ya kuanzisha zoezi hilo ifanikiwe na baada ya miaka mitano tija ianze kupatikana.