NA MWANDISHI WETU, DODOMA
IDADI ya wagonjwa wa afya ya akili waliopatiwa huduma kwenye Hopitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe imeongezeka kutoka 79,619 katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi, 2022 hadi kufikia 138,625 kati ya Julai 2022 na Machi, 2023.
Akiwasilisha mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2023/24, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi, 2023 hospitali ilihudumia wagonjwa 212,065, kati yao wagonjwa 138,625 sawa na asilimia 65.3 walikuwa wagonjwa wa afya ya akili.
Amesema kati ya Julai 2021 hadi Machi 2022, wagonjwa waliohidumiwa katika hospitali hiyo walikuwa ni 131,711 ambapo kati yao wagonjwa 79,619 sawa na asilimia 60.4 walikuwa wagonjwa wa afya ya akili. Amesema katika wagonjwa 104,400 walikuwa wagonjwa wa nje na wagonjwa 107,665 walikuwa ni wagonjwa wa kulaza katika kipindi cha kati ya Julai 2022 hadi Machi, 2023.
“Huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ambazo zimetolewa na hospitali ni magonjwa ya mfumo wa fahamu, magonjwa ya kumbukumbu, saikolojia, magonjwa ya afya ya akili, huduma za afya ya akili kwa watoto na vijana, magonjwa ya wanawake, mifupa na watoto,”amesema.
Ummy amesema katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, hospitali hiyo imeendelea kutekeleza huduma za mkoba, ambapo jumla ya wanafunzi 18,154 walipatiwa elimu kuhusu magonjwa ya afya ya akili katika shule 99 mbalimbali za sekondari mkoani Dodoma.
Aidha, amesema hospitali imeendelea kuboresha huduma za afya ya akili kwa kutoa elimu kwa jamii na matembezi na kufanikiwa kuwafikia Watanzania 25,564 katika Mkoa wa Dodoma.