NA EDNA BONDO
SURA ya 95 ya Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa kazi, 2003 inamtaka Mwajiri kutoa mazingira yenye afya na salama kwa wafanyakazi na kufidia wafanyakazi walioathirika kiafya kutokana na mazingira ya kazi.
Sehemu ambayo vitu vyenye sumu vinazalishwa, kutunzwa au kuhifadhiwa,
Mkaguzi mkuu wa masuala ya afya anaweza kumtaka mwajiri kutoa huduma za ziada kama Maliwato ya kuogea, kuandaa uchunguzi wa mara kwa mara wa afya toka kwa taasisi inayokubalika ikiwa ni pamoja na kutoa mavazi ya kujikinga.
Kutokana na Mwajiri kutakiwa kuzingatia haya na mengine mengi mahali pa kazi hususani hapa nchini kwetu Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo angalau zimeweza kupiga hatua katika hilo.
Na kupiga kwake hatua kumetokana na shuhuda za wenzetu kutoka nchi jirani ambao wanapokuja Tanzania hujionea jinsi usalama mahali pa kazi unavyozingatiwa.
Wawezeshaji wa haya yote ni Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), ambao hutoa mafunzo na ufuatiliaji wa karibu katika Taasisi mbalimbali na iwapo sheria zitakiukwa basi hatua husika huchukuliwa ili kuhakikisha Mwajiriwa analindwa.
Siku kadhaa zilizopita ujumbe wa wataalamu kutoka Wizara ya Kazi na Hifadhi ya Jamii kutoka Kenya umehitimisha ziara yake ya siku nne nchini iliyolenga kubadilishana uzoefu kuhusu sheria na taratibu mbali mbali za kazi.
Katika ziara yao ya kubadilishana uzoefu wajumbe wa ziara hiyo wamesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika usimamizi wa masuala ya kazi hususan mifumo ya usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha ziara yao katika Ofisi za OSHA, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi ya Kenya, Geoffrey Kaituko, anasema nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikitafuta uzoefu wa mambo mbali mbali ughaibuni ilihali uzoefu huo unapatikana katika nchi zinazowazunguka.
“Ziara yetu hapa Tanzania imekuwa ya kufana sana, tumetembelea Taasisi mbali mbali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Kwahiyo sisi tumefurahi sana kwa mapokezi mazuri tuliyoyapata pamoja na mambo mazuri tuliyojifunza.”amesema Kaituko na kuongeza kuwa
” Mara nyingi tumekuwa na mazoea ya kwenda Ulaya kujifunza mambo fulani fulani mfano kwa mambo haya ya OSHA tungetaka kwenda Ujerumani wakati hapa Tanzania kuna Taasisi nzuri sana inayosimamia masuala ya usalama na afya hivyo jambo ambalo tunatoka nalo hapa ni kwamba nasisi ni lazima twende tukaanzishe Taasisi kama hii,”
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Jamal Katundu, anasema kupitia ziara hiyo ya wataalam kutoka Kenya, Ofisi yake imejifunza mambo mengi ikiwemo jinsi walivyofanikiwa kuwezesha watu wao kupata ajira nje ya nchi yao na hivyo kuliingizia Taifa lao fedha nyingi za kigeni.
“Mfano katika suala la Wakenya wanaofanya kazi nje yan chi yao, Saudi Arabia wana wafanyakazi zaidi ya 120,0000, Qatar zaidi ya wafanya kazi 60,000 na nchi nyingine za Kiarabu zaidi ya 40,000 hivyo nimejifunza kwamba fedha wanayopata kutoka nje kutokana na ajira za nje ni zaidi hata ya fedha zinazotokana na mazao yao makuu ya biashara kama vile Kahawa na Chai.”
” Nimemwelekeza Mkurugenzi anayehusika na Huduma za Ajira aangalie ni kwa jinsi gani tunaweza kujifunza kutoka kwa wenzetu ili nasi tuweze kunufaika na ajira za nje ya nchi,” ameeleza Prof. Katundu.
Wakati huo huo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, anasema ziara hiyo inafungua ukurasa mpya wa ushirikiano hususan kwenye eneo la sheria na taratibu mbali mbali za kazi baina ya OSHA Tanzania na Kenya jambo ambalo litakuza uwekezaji baina ya nchi zote mbili pamoja na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa sera ya soko la pamoja la Afrika Mashariki.
“Tumekuwa na mazungumzo mazuri sana, tumejifunza kutoka kwao na wamejifunza kutoka kwetu lakini tunafahamu kuwa sisi ni Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika Jumuiya hii kuna kitu kinaitwa Soko la Pamoja (Common Market) na kuna wawekezaji wa Tanzania huko Kenya na wao wapo hapa kwetu. Hivyo ni muhimu sana kwa nchi hizi kuwa na ulinganifu wa sheria mbali mbali ili kuwezesha uwekezaji na biashara kufanyika katika mazingira mazuri,” anabainisha Mtendaji Mkuu wa OSHA.
Naye Mkurugenzi wa Masuala ya Usalama na Afya katika Wizara ya Kazi Nchini Kenya, Dk.Musa Nyandusi, anasema wapo mbioni kuunda Taasisi Mahsusi kwa ajili ya kusimamia masuala ya Usalama na Afya nchini kwao ili kuendana na miongozo ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) hivyo wanatarajia kujifunza mengi kutoka Tanzania ambayo imepiga hatua kubwa katika usimamizi wa masuala husika.
Taasisi ya OSHA ilianzishwa rasmi Agosti 31, 2001 ikiwa ni jitihada za serikali ya Tanzania ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, kiteknolojia pamoja na kukidhi matakwa ya Mikataba ya Kimataifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO ) inayozitaka nchi wanachama kuwa na chombo mahsusi cha kusimamia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.



