NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Tume ya Maboresho Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) makao makuu, umetangaza kujiuzulu.
Taarifa iliyotolewa Aprili 30, 2023 na aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo, Sheikh Issa Othman Issa ilieleza kuwa pia wajumbe wanne wa tume hiyo wamejiuzulu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kuna sintofahamu na ugumu katika kutekelezji wa majukumu waliyokabidhiwa.
Shehe Issa alidai kuwa walishindwa kufikia malengo yaliyokabidhiwa kutokana na kukosa muda wa kutosha na umakini wa kusimamia majukumu hivyo kuwafanya washindwe kuendelea na kufikia uamuzi huo.
Wajumbe wengine waliojiuzulu ni Mohammed Nyengi, Daudi Nassib na Iddi Kamazima, na Omar Igge.
Kujiuzulu kwa wajumbe hao kunaifanya tume hiyo ibaki na wajumbe wawili ambao ni Alhaj Nuhu Mruma na Shehe Qassim Jeizan.
Aliyekuwa Katibu wa tume hiyo, Sheikh Igge alisema wamejiuzulu kutokana mazingira magumu waliyokuwa wakikumbana nayo katika kutekeleza majukumu yao.
“Kwa mujibu wa hadidu rejea za kuundwa kwa tume, ya kwanza kabisa tulipewa kazi ya kuhakiki madeni na kushauri namna bora ya kuyalipa, sasa imetuwia vigumu kufanya huo uhakiki kwa sababu huwezi kufanya uhakiki bila kufanya ukaguzi na tumekuwa tukiwekewa ugumu wa kufanya ukaguzi,” alidai Sheikh Igge.
Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir aliunda tume hiyo Januari 20 mwaka huu na kupewa hadidu za rejea zilizowaelekeza kwanza kuhakiki madeni ya Bakwata na kushauri namna nzuri ya kuyalipa na kufanya uchunguzi wa mali za Bakwata zinazomilikiwa na watu wengine kinyume na utaratibu na kuwachukulia hatua.
Pia Tume ilielekezwa kufanya tathmini ya changamoto za mifumo ya utawala inayokabili taasisi hiyo na kushauri namna bora ya kufanya maboresho, kufanya uchunguzi wa mikoa au wilaya yenye migogoro mikubwa ya uongozi au mali na kuchukua hatua za kuitatua na masuala mengine ambayo tume itaona yanafaa kufanyiwa kazi.