NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KATIKA kuendelea kurudisha mchango wake kwa jamii watumishi wa Hoteli za Hyatt Regency wameendesha zoezi ya uchangiaji damu katika kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji katika hospitali zilizopo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Meneja Mkuu wa Hoteli ya Hyatt Regency Alexander Eversberg alisema suala la kurudisha kwa jamii ni kutokana na huduma wanazotoa kwa kuchangia damu salama kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wateja wao pamoja na wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali.
Alisema ifikapo mwezi Aprili kila mwaka, Hoteli zote za Hyatt Regency hurudisha kwa jamii kwa kufanya shughuli mbalimbali ambazo zinagusa moja kwa moja jamii ikiwemo kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya mji,kutoa msaada kwa vituo vya watoto yatima au kuchangia damu
Wakati huo huo Ofisa wa Rasilimali Watu Hoteli ya Hyatt Regency Iddah Mushi alisema kwa kuwa wamekuwa wakiwasiliana na watu wa benki ya damu salama, wameona kumekuwa na uhaba mkubwa wa damu na uchangiaji ni mdogo kwa hiyo wameona kushirikiana na wadau wengine ili kufanya zoezi hilo ili kugusa jamii mmoja mmoja
Kwa upande wake Ofisa Uhamasishaji Mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Mashariki Mary Meshi ameipongeza Hyatt Regency kwa kutambua kutoa damu ni sehemu ya maisha ya kila mmoja na kuamua kutoa sehemu ya kurudishia katika jamii.
“Tumekuwa na uhitaji mkubwa wa damu hivi karibuni kutokana na waau muhimu wa uchangiaji damu kuwa katika shughulli za mfungo kwahiyo Hyatt kujitokeza na kuweza kusaidia hili katika ukusanyaji wa damu kwetu sisi ni faida”. alieleza
Aidha alitoa wito kwa Ofisi na Taasisi zingine kuendelea kuchangia damu ili kuweza kuokoa maisha ya watu wengine kwani hatuwezi kupata damu salama bila jamii kujitoa kwa moyo kuchangia damu.