NA MWANDISHI WETU, SHINYANGA
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamelalamikia hatua ya zahanati ya Kijiji cha Bugogwa iliyopo kata ya Mwamala kufungwa kwa muda wa mwaka mmoja, kutokana na kukosa watumishi wa afya.
Diwani Viti Maalum, Anna Pius ametoa ripoti hiyo leo Aprili 28, 2023 kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani cha robo ya tatu ya mwaka na kujadiliwa na madiwani wote na kutaka Mkurugenzi Nice Munisy aeleze kuhusu jambo hilo.
Pius ameeleza kufungwa huko kulitokana na daktari aliyekuwepo kwenye zahanati hiyo kufariki na kubaki muuguzi peke yake ambaye alidai hawezi kuwapa huduma wala kujaza madokezo.
“Wananchi sasa hivi wanapata huduma kwenye zahanati ya Kijiji cha Mwamala na kituo cha Afya Samuye,”amesema Pius.
Diwani wa Kata ya Itwangi, Sonya Mhela, amesema taarifa hiyo waliipata kutoka kwa wananchi wa eneo hilo na kuanza kufuatilia na kugundua kituo kimefungwa.
Diwani wa Kata ya Salawe na Kata ya Ilola Amos Mshandete, wamesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitafuta fedha ili kuwaondolea changamoto wananchi kupata huduma za afya, lakini ni aibu zahanati kufungwa na watoto wamekuwa wakisumbuka kupata chanjo.
“Tunaomba mganga mkuu wa halmashauri atuombe radhi baraza kwani taarifa hii Mkurugenzi amedai haifahamu, ikiwa kila siku inatakiwa kuripoti taarifa kwa mkurugenzi afahamu na achukue taarifa,”amesema Mshandete.