NA MWANDISHI WETU, TANGA
KATIKA kusherehekea maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amezindua jengo la maabara ya umeme katika shule ya kijeshi ya ulinzi wa anga.
Amesema kuwa uwepo wa maabara hiyo utasaidia kwa kiwango kikubwa kuongeza ubunifu kwenye masuala ya tafiti za kisayansi katika umeme.
“Ni imani yangu uwepo wa maabara hii utaongeza chachu ya kujifunza na ugunduzi wa masuala ya kiufundi katika umeme, lakini na kuja na teknolojia ya kudhibiti athari zinazosababishwa na umeme pindi unapoleta hitilafu usiweze kuleta majanga katika vifaa vinavyotumia umeme,”amesema RC Kindamba.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Kijeshi ya Anga, Kanali Abel Mbai amesema kuwa maabara hiyo imegharimu Sh.Mil 221 na itatumiwa na wanafunzi wa kijeshi wanaosomea fani ya umeme.
“Uwepo wa maabara hii ya umeme unakwenda kuongeza ufanisi katika mafunzo kwa vitendo, lakini na kuwajengea uwezo na weledi wa kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya umeme,”amesema Kanali Mbai.