NA MWANDISHI WETU, MBARALI
WATU wanne wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za jadi wameteka magari matatu eneo la mlima Mwami Kata ya Mswisi wilayani Mbarali katika barabara kuu ya Tanzania na Zambia (Tanzam) usiku wa kuamkia leo Aprili 26,2023.
Akizungumza leo Jumatano Aprili 26,2023 Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Denis Mwila amethibitisha kutokea tukio hilo na kwamba limetokea saa 8.30 usiku.
“Majambazi hao baada ya kufanikiwa kusimamisha magari hayo walifanya uharibifu kwenye vioo vya mbele kwenye magari mawili likiwepo basi la abiria ambayo yote yalikuwa yakitokea Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwenda Jijini Dar es Salaam.”amesema
Ameongeza kuwa “baada ya kufanya uharibifu huo ndipo waliokwenda kwenye gari ndogo lililokuwa likisafirishwa (IT) na kupora dola za Marekani 200 (Sh.430,000) na fedha za kitanzania 150,000 (jumla Sh.580,000)”
Kanali Mwila amesema taarifa za awali zimebaini gari lililotumiwa na majambazi hao ni aina ya Toyota Noah ambayo inaendelea kufuatiliwa ili kubaini watu waliohusika na tukio hilo.
”Tunashukuru Mungu hakuna mtu aliyepata madhara kutokana na tukio hilo kwa sasa tumeliachia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuchukua hatua zaidi sambamba na kuona ya kuimarisha usalama kwa mabasi na magari ya masafa marefu,”amesema.
Mkazi wa Mswisi ,Jane Joel kuwa eneo hilo ni hatari sana nyakati za usiku na kuomba Serikali kuweka utaratibu wa kusindikiza mabasi na magari madogo yanayofanya safari za usiku.