NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewaonya wakazi wanaoishi mabondeni kuchukua tahadhari kwani kutashuhudiwa vipindi vikubwa vya mvua kwa muda wa siku mbili kuanzia Aprili 22, 2023 na Aprili 23, 2023.
Aidha TMA imetabiri kunyesha kwa mvua kubwa katika mikoa mitatu nchini ikiwemo, Pwani na Zanzibar
TMA imefafanua kuwa vipindi hivyo vya mvua vitashuhudiwa kwa siku mbili mfufulizo katika Jiji la Dar es Salaam, mikoa ya pembezoni na mkoani Morogoro.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Ladislaus Chang’a amesema wanaoishi mabondeni wanapaswa kuchukua tahadhari
Amesema mvua zinazoendelea sasa ni utabiri uliofanyika Februari 22, mwaka huu ambapo TMA ilitabiri Dar es Salaam, Pwani, Zanzibar na Mororgoro zingepata mvua za juu kuliko kawaida.
“Wakazi wanapaswa kujitayarisha kwa baadhi ya siku za mvua za juu ya kawaida, ambazo zinaweza kuwa na athari kwa usafiri na maji pia kuna uwezekano wa kutokea kwa hali mbaya ya hali ya hewa ambayo inatarajiwa kuathiri usafiri na miundombinu,” amesema.
Kwa mujibu wa kaimu mkurugenzi huyo, baadhi ya maeneo yatatarajiwa kuzungukwa na maji, uharibifu wa miundombinu ambayo inaweza kuathiri shughuli za kiuchumi.
Dk Chan’ga amesema wataendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa kwa wananchi ili waendelee kuchukua tahadhari.