NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATCL) linakusudia kuingia makubaliano na Shirika la Ndege la Ndege Kenya (KQ) ya kushirikiana katika usafirishaji wa mizigo.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Jumatano, Aprili 19, 2023 imeeleza kuwa lengo jingine na makubaliano hayo ni kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa kampuni hizo.
Wakizungumza katika kikao cha awali na viongozi wa ATCL, Mtendaji Mkuu wa KQ, Allan Kilavuka amesema wamelazimika kufanya hivyo kutokana na uwepo wa maeneo mengi ambayo KQ na ATCL zinaweza kushirikiana.
Kilavuka amesema Kenya ni kituo cha usafirishaji mizigo katika bara la Afrika na kutokana na hali hiyo wanaweza kuingia makubaliano na Tanzania kuhakikisha ndege mpya ya mizigo Boeing 767-300 yenye uwezo wa kubeba tani 54 kwa mara moja, inatumika kikamilifu.
“Hivi karibuni Tanzania itapokea ndege yake ya mizigo itakayoweza kutatua changamoto ya usafirishaji mizigo kwa kiwango kikubwa. Tunaamini tunaweza kushirikiana kwenye eneo hili,” amesema Kilavuka.
Siku chache zijazo ATCL inatarajia kupokea ndege ya mizigo yenye uwezo wa kubeba mizigo hadi tani 3,000 kwa mwaka na kuondoa adha ya wafanyabiashara wanaopeleka mizigo yao nje ya nchi.
Kilavuka amesema KQ na ATCL wanaweza kushirikiana katika kusafirisha abiria kwa kuzingatia misingi yenye kunufaisha pande zote mbili.
“Kupitia ndege tulizonazo, vifaa na wataalamu wetu wakitumika ipasavyo tutaongeza thamani na kupunguza gharama za uendeshaji wa ATCL na KQ. Uwepo wa ndege ya Boeing 787- 8 (Dreamliner) na ujio wa ndege ya mizigo Boeing 767- 300F zinafungua fursa zaidi za kibiashara,” amesema Kilavuka.
Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema kikao hicho kilichofanyika makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam, kimeangalia masuala yatakayosaidia ustawi wa taasisi hizo, kuzingatia mahitaji makubwa katika soko la dunia