NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SERIKALI imeagiza viongozi wa vyama vya siasa waendele kutembelea miradi ya kimkakati.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema hayo Dar es Salaam Aprili 16, 2023 wakati akifungua mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa.
Mhagama alisema kila chama kina itikadi yake lakini huenda wana ushauri mzuri zaidi kwa serikali kuhusu masuala ya ustawi wa nchi hivyo viongozi wa vyama vya siasa lazima wapate fursa ya kushauri.
Alisema serikali imekuwa ikipata ushauri wa viongozi wa vyama vya siasa na ukiwasikiliza unaweza kupata mambo ya msingi yenye manufaa kwa nchi.
“Tunapofika kwenye suala la uchumi na maendeleo ya taifa hakuna vyama. Kuna kila sababu viongozi wa vyama vya siasa, Baraza la Vyama vya Siasa lipate nafasi ya kuangalia hiyo miradi ya kimkakati ambayo ni ya ustawi wa nchi nzima..na wakati mwingine kushauri ni kuona kinachoendelea”alisema na kuongeza;
“Mwisho wa siku ni Tanzania yetu, mwisho wa siku si chama ni ustawi wa taifa letu. Na kwa kila kila kiongozi wa chama mwenye nia na maono mazuri kwa taifa hili ni lazima yapo mambo lazima yatuunganishe…yapo mambo ambayo tupende tusipende yanatuunganisha kama Watanzania”.
Alisema kuna haja ya kutengeneza programu za mafunzo kwa viongozi wa vyama vya siasa kwa kuwa dunia inabadilika na sasa kuna mapinduzi ya nne ya viwanda.
Alisema Tanzania haiwezi kuwa na demokrasia imara kama viongozi wa vyama vya siasa hawaendani na kasi ya mabadiliko kwenye ulimwengu wa sasa na mazuri yote ya baraza hilo yatangazwe.
Mhagama amemuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa ahakikishe baraza hilo linapata fursa ya kutosha kukutana na kujadiliana na serikali kuhusu masuala yanayohusu ustawi wa demokrasia nchini.
Alisema baraza hilo likihitaji kukutana na viongozi kama si Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu wapate fursa hiyo bila kikwazo.
“Tutaendeesha uchumi vizuri wa nchi, tutasimamia miradi ya kimkakati vizuri kama tutakuwa na maoni ya wanasiasa. Wanasiasa ni kundi muhimu, ndio wanaojua mahitaji ya wananchi”alisema
Alieleza kuwa kwa mara ya kwanza serikali imeweka fungu maalumu na kutenga shilingi 1,586, 662, 000 kwa ajili ya kuendesha shughuli za Baraza la Vyama Vya Siasa.
Ameagiza vikao vyote vya kikatiba vya baraza vikiwamo vya baraza vifanyike na wajumbe wasikopwe.
Lakini pia alitaka baraza hilo likubali kukoselewa linapofanya vibaya na pia sheria za matumizi na mapato ya fedha zizingatiwe ili kuepuka taarifa mbaya za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG ) kuhusu matumizi ya fedha kwenye vyama.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema migogoro ya kisiasa ndani ya vyama ipo kwa sababu kuna watu wanakuwa na malengo tofauti ndani ya vyama vya siasa.
Profesa Lipumba alisema wapo wanaohitaji kupata umaarufu na wengine uongozi bila ya kufuata utaratibu ilani muhimu ii migogoro iweze kutatuliwa kwa njia ya demokrasia na kuleta kutokuwa na ugonvi.
“Huwezi ukawa ndani ya siasa pakawa pametulia, ukadhani upo msibani. Lazima patakuwa na shughuli ambazo zitakuwa zikigonga vichwa ” alisema