NA MWANDISHI WETU, BUCHOSA
WAKAZI wa Kata ya Katwe wilayani hapa mkoani Mwanza wameanza ujenzi wa Shule ya Msingi Mlimani ili kuondokana na mrundikano wa wanafunzi shuleni hapo.
Aidha ujenzi huo unakwenda sambamba na ongezeko la idadi ya wanafunzi katika shule ya msingi Kahunda yenye zaidi ya wanafunzi 2000.
Akizungumza na Demokrasia , Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Buchosa na Diwani wa Kata ya Katwe Max Mkungu amesema hapo awali iliwalazimu wanafunzi wengi kuwa watoro na wengine kukatiza masomo yao njiani kwa sababu ya kutembea umbali mrefu na hivyo kusababisha kushuka kwa kiwango cha elimu kwenye kata hiyo
Ujenzi huo ambao umekuwa ukifanyika kila alhamisi ya wiki kwa kushirikisha wananchi wote 15000 wa kata hiyo.
Alisema kuwa pindi tu ujenzi huo utakapokamilika utasaidia kuinua kiwango cha elimu wilayani hapo.
“Mbunge alifika hapa na tulifanya shughuli za maendeleo lakini pia Halmashauri imeona jitihada za watu hawa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2023 na 2024 ambayo bunge limeanza kujadili hivyo wameomba walau kwenye hii shule ipewe milioni mia mbili kutoka kwenye serikali kuu” alisema.
Mkungu alisema ujenzi huo ambao kwa sasa una vyumba vitatu vya madarasa na matundu sita ya vyoo aliitaka serikali na watanzania wote wenye moyo uzalendo kuelendelea kuchangia ujenzi wa shule hiyo chini ya kauli mbiu yao “Tukishirikiana kwa pamoja Katwe inasonga mbele”.
Mbali na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kufungulia mikutano ya hadhara pia aliwataka wapinzani kunadi sera zao na kufanya siasa za kistaarabu.
Kwa upande wao wanafunzi wa Shule hiyo ya Mlimani, Mariam Masanja alisema wamefuraia sana ujenzi wa shule na kuahidi kusoma kwa bidii ikiwemo kushika nafasi za juu kwenye mitihani yao ya kitaifa.