NA ANDREW CHALE,DAR ES SALAAM.
RAIS Mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chisano amesema kuwa alijifunza lugha ya Kiswahili mitaa ya Kariakoo jijini Dar es salaam akiwa nchini Tanzania wakati wa harakati za uhuru wa nchi hiyo.
Chisano ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya usiku wa utoaji tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu alisema kuwa akiwa maeneo mbalimbali ya Tanzania wakati, huo aliweza kujifunza lugha hiyo ya Kiswahili hasa eneo la Kariakoo pia katika maeneo mengine ya makazi wakati huo wakiwa kwenye harakati.
“Kuna mtu amesema amejifunza Kiswahili cha mtaani, mimi pia nimejifunza Kiswahili nikiwa Kariakoo.
Nimeweza kupunguza maeneo mengi ya Tanzania na kuishi huko”.
Amesema alikaa na kufanya kazi maeneo mengi ya Tanzania lakini pia alipokuwa Rais na mwenyekiti wa AU alipendekeza watumie Kiswahili, aliongea na Rais Benjamin Mkapa wakati ule, lakini Museven na marais wa Kongo na Burundi juu ya kutumia Kiswahili, na walikiasisi na wanajivunia hadi leo Kiswahili kimekuwa
Katika tukio hilo ameweza kusoma hotuba yake kwa Lugha ya Kiswahili huku akikumbushia namna alivyopambana harakati za uhuru kutokea Tanzania.
Katika hatua nyingine, amezitaka nchi za Afrika Mashariki kuendeleza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika maeneo muhimu ya kiutawala na kijamii.
Amesema, Kiswahili ni lugha yetu ya Afrika hivyo hakuna budi kuilinda na kuikuza kwa kuipa heshima na dhima mbalimbali mathalani kutumika katika elimu, siasa, utawala na masuala mengine ya kijamii.
“Ninatoa wito kwa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Mabaraza ya Kiswahili ya nchi wanachama kuendeleza matumizi ya Kiswahili katika maeneo muhimu ya kiutawala na kijamii kwani Kiswahili ni tunu na utambulisho wa Afrika na Mwafrika.”amesisitiza
Aidha Chisano, ameipongeza Tanzania kupitia kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa kuenzi, kuiendeleza, na kuikuza lugha adhimu ya Kiswahili kupitia shindano la uandishi bunifu.
“Kama tujuavyo, lugha ya Kiswahili ina historia kubwa katika ukombozi wa bara la Afrika. Vilevile, lugha ya Kiswahili ni lugha rasmi katika Umoja wa Afrika na inazungumzwa takribani katika mabara yote.
“ Hivyo, utoaji wa Tuzo za Ubunifu ni kuendelea kutambua thamani muhimu kabisa ya lugha ya Kiswahili hapa nchini na Afrika kwa ujumla. Hongera sana Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan.”amesema
Rais Chisano pia, amewapongeza Watanzania, kwa kutambua na kuenzi mchango wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kukuza lugha ya Kiswahili.
“Ni wazi kabisa Mwalimu Nyerere kwa dhati kabisa, aliikuza lugha ya Kiswahili kwa kuandika maandiko bunifu kama mashairi, riwaya na kutafsiri kazi mbalimbali za fasihi ya Kiingereza katika Kiswahili. Hivyo, ni heshima kubwa tuzo hii kupewa jina la Mwalimu Nyerere.
“Pia, ni fahari kubwa kwangu kupata heshima ya kuwa mgeni rasmi katika halfa ya tuzo hii ya mwaka 2023.”amesema
Amesema, Kiswahili nyumbani kwake ni Tanzania; hivyo, juhudi kama hizi za kutambua mchango wa wadau wa maandiko bunifu kwa lugha ya Kiswahili ni kitu muhimu sana.
“Ni maoni yangu kuwa juhudi hizi ziendelezwe bila ukomo kwani uhai wa lugha yoyote iwayo duniani, ni kuwapo na machapisho yaliyoandikwa kwa lugha hiyo”
Aidha, katika tuzo hizo, washindi 10 waliweza kupatikana ikiwemo wa Mashairi na wa Riwaya.
Mshindi wa kwanza wa Riwaya ilienda kwa Hamisi Kibari ambaye pia ni Mhariri wa gazeti la Serikali la HabariLeo
Kibari ameshinda kupitia riwaya yake ya ‘Gereza la Kifo’ ambapo amezawadiwa shilingi millioni 10, Ngao, Cheti na kuchapishiwa mswaada wake “Gereza la Kifo’ ambao pia utasambazwa mashuleni.
Upande wa mshindi wa kwanza wa shairi umeenda kwa Amri Abdalah kupitia kitabu chake cha ‘Mtale wa Ngariba’.
Rajabu amezawadiwa shilingi Milioni 10, Ngao, Cheti na kuchapishiwa mswaada wake na kusambazwa mashuleni.
Aidha, washindi wengine wameweza kupata vyeti maalum vya kutambua ushiriki wao.