NA FARIDA RAMADHANI, DODOMA
SERIKALI imeeleza kuwa hakuna mikopo ambayo imeshindwa kulipa katika kipindi cha Awamu zote sita za uongozi.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Chande alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bunda, Boniphace Getere aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kupata mkopo wa fedha nyingi wa muda mrefu kwa masharti nafuu ili kulipia madeni sumbufu katika Awamu zote sita (6).
Chande amesema katika kipindi cha Awamu zote sita (6) Serikali imeendelea kukopa na kulipa mikopo kulingana na mtiririko wa malipo kwa kila mkopo na hakuna mikopo ambayo Serikali imeshindwa kulipa.
“Malipo ya madeni yote ikiwemo madeni sumbufu yanaendelea kulipwa kupitia mpango na bajeti za Serikali za kila mwaka”, amefafanua Chande.
Amesema Serikali inaendelea kusimamia deni la Serikali kupitia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134 inayobainisha vigezo vya kuzingatia wakati wa kutafuta fedha za mikopo kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli za Serikali, hususani miradi ya maendeleo.
Amebainisha kuwa Sheria hiyo pia inatumika kama nyenzo ya kudhibiti ongezeko la deni la Serikali kwa kulipa mikopo iliyoiva na kutoa kipaumbele kwa mikopo yenye masharti nafuu.