NA MWANDISHI WETU, IRINGA
UCHUNGUZI wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa umemnasa mmoja wa wamiliki halali wa silaha anayetuhumiwa kujipatia fedha kutoka kwa magenge ya uhalifu kwa njia ya kuzikodisha
Taarifa iliyotolewa Aprili 11, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Allan Bukumbi imesema mtuhumiwa huyo (jina lake limehifadhiwa) alikamatwa Aprili 3, mwaka huu majira ya Saa 11:30 katika eneo la Kihesa Kilimani, mjini Iringa.
ACP Bukumbi alisema mtuhumiwa ametajwa kukodisha silaha zake hizo aina Shortgun na Rifle pamoja na risasi zake kwa Sh.100,000 kila moja katika kila tukio la uhalifu jambo ambalo ni kinyume na sheria na utaratibu wa matumizi ya silaha.
“Tunakamilisha upelelezi na wakati wowote kuanzia sasa tutamfikisha mahakamani kujibu tuhuma hizo,” alisema na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi lao kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu katika maeneo yao.
Katika tukio jingine, Bukumbi alisema jeshi lake linaendelea kumsaka Rashid Nyomolelo anayetuhumiwa kuiba silaha aina ya Pistol Rami pamoja na risasi zake 10 mali ya Joseph Lukonde (44) iliyosalimishwa Aprili 4, mwaka huu karibu na nyumba ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwangata A mjini Iringa.
Aidha Kamanda Bukumbi alisema Polisi imemtia nguvuni Amani Kasisi (47) mkazi wa Nzihi wilayani Iringa anayetuhumiwa kumlawiti na kumsababishia maumivu makali sehemu za haja kubwa mtoto wake mwenye mwaka mmoja na miezi kumi.
Wakati huo huo jeshi la Polisi limetangaza kuanza kuyachunguza mashirika yasio ya kiserikali yanayofanya kazi zake mkoani Iringa ambayo hivi karibuni kwa kupitia ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Dk Harrison Mwakyembe yametuhumiwa kujihusisha kuchochea vitendo vya ushoga na usagaji.
“Tumeipokea taarifa ya Dk Mwakyembe kama tunavyopokea taarifa zingine za matukio ya uhalifu. Tayari tumeanza kuyahoji mashirika yanayofanya kazi mkoani Iringa yaliyotajwa katika ripoti hiyo na kazi hiyo tunaendelea nayo ili kama yatabainika kuhusika basi mkono wa sheria ufuate juu yao,” alisema.