NA TATU MOHAMED, DAR ES SALAAM
SERIKALI, Kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wanawake na Makundi maalum imedhamiria kuimarisha utoaji wa huduma za ustawi wa Jamii katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii iliyopo jijini Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Wakili Amon Mpanju wakati wa ziara yake chuoni hapo Aprili 06, 2023 alipokutana na menejimenti ya Chuo hicho.
Uamuzi huo wa Serikali umefuatiwa baada ya Mkuu wa Chuo kutoa taarifa ya namna ambavyo chuo hicho Kinatoa huduma za ushauri na jinsi kinavyoshirikiana na Jamii kwa ujumla kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Wakili Mpanju amekipongeza Chuo cha Ustawi wa Jamii kwa ufanikishaji wa huduma ya elimu na msaada wa kisaikolojia kwa wananchi, mashirika na taasisi mbalimbali binafsi na za serikali.
“Kazi mnayoifanya ni nzuri na ni kubwa ,nilichopenda zaidi ni vile mlivyobadilika na kukidhi mahitaji ya vijana kwasababu mlikua kitaaluma zaidi lakini sasa mmekua na programu ya ushiriki jamii.Hiyo inaonesha umuhimu wa taasisi hii katika kutatua changamoto za kijamii” amesema Mpanju
Katika hatua nyingine Wakili Mpanju amesisitiza uboreshaji wa huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ndani ya Chuo cha Ustawi wa Jamii huku akitoa ahadi ya Serikali yakupeleka wataalam wa lugha ya alama kutoka wizarani.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Baraka Makona amesema kuwa atasimamia utekelezaji wa yote waliyokubaliana kati ya Wizara na Menejimenti ya Chuo ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa shughuli za Taasisi
“Tunataka Taasisi hii kwa misingi ya mahitaji kama vile kuchapisha vitabu vya wasioona kuwepo na mashine hapa ambayo tutakua tunatumia” amesema Makona
Naye Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dk.Joyce Nyoni ametoa shukrani na pongezi kwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwaajili ya maendeleo ya Taasisi pamoja na kuwapatia Kibali cha kuajiri watumishi wapya 52 ambao wataongeza ufanisi ķatika Kufundisha.