NA JANET JOVIN, DAR ES SALAAM
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Ndaki ya Sayansi za Jamii kimeiomba Serikali kuhakikisha jamii zinazozunguka hifadhi mbalimbali za taifa zinanufaika na maliasili hizo.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam Aprili 5, 2023 na Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii, Profesa Christine Noe wakati wa uzinduzi wa kitabu kuhutimisha mradi wa ’Ushirikiano wa wadau mbalimbali katika Uhifadhi na Maendeleo ya Kiikolojia na Jamii. (NEPSUS).
Prof.Noe amesema katika kitabu hicho ambacho utafiti wake ulijikita kwenye maliasili, misitu na mazao ya bahari, ulibani kuwa licha ya ongezeko la shughuli za kuhifadhi maliasili bado wananchi wanaozunguka hifadhi hizo hawajaweza kunufaika.
Amesema ni muhimu sasa kwa serikali kuhakikisha jamii zinazozunguka maliasili hizo zinanufaika ili ziweze kubadilisha hali zao za kiuchumi.
“Katika kitabu tumeangalia upande wa jamii zinazopatikana karibu na misitu, tumeeleza namna ambavyo zinavyoweza kunufaika na uwepo wa maliasili zinazowazunguka, tunaomba utafiti huu uwafikie ili kuweza kubadilisha hali ya kiuchumi za wananchi hao,” amesema na kuongeza
“Machapisho ya kitaaluma tumefanya sasa yapo kwenye sehemu zinazotakiwa za kitaaluma lakini mapendekezo ya serikali nini ifanye, tulitafuta wadau wa maliasili, wakurugenzi wa misitu na uvuvi tukajadiliana nakuja na mapendekezo madogo ya kisera ili serikali uweze kubadilisha sera kulingana na maisha ya sasa” amesema
Kwa upande wa mhariri wa kitabu hicho, Dan Brockington kutoka Chuo Kikuu cha Autonomous Barcelona amesema kuwa walifanya utafiti na kuja na kitabu hicho kwa ushirikiano mkubwa kati yao na UDSM.
“Tanzania inabahati ya kuwa na watafiti wengi wanaofanya kazi zao katika usimamizi wa maliasili kwahiyo imekuwa ni rahisi kwetu kufanya utafiti huu juu ya misingi mizuri ambayo ilikuwa imejengwa tayari.” amesema Brockington
Amesema changamoto kubwa ni kulinganisha chanzo cha mapato kwa wananchi ni tofauti na maliasili inayopatikana katika eneo husika hivyo ameshauri kuwa eneo la hifadhi ya maliasili likiongezeka basi na kipato cha wananchi kiwe kizuri.
Kwa upande wake mhariri Stefano Ponte kutoka Shule Kuu ya Biashara ya Copenhagen, amesema kuwa ushirikiano katika utafiti huo ulianza 2016 hadi 2020 ingawa yeye alikuwa na mawazo mengine katika utafiti huo.
Amesema waliungana pamoja katika utafiti huo na sasa wanasheherekea uzinduzi wa kitabu hicho pamoja hivyo hio ni hatua kubwa kwani hata yeye amejifunza mengi kupitia utafiti huo.
