NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
BENKI ya NMB imetoa msaada wa vifaa mbalimbali katika sekta ya afya na elimu katika halmashauri tatu za Mlimba, Malinyi na Manispaa ya Morogoro ikiwa sehemu ya benki hiyo kurejesha faida kwa jamii baada ya mwaka 2022 kupata faida ya kiasi cha sh.bilioni 429 huku ikitenga kiasi cha sh.bilioni 6.2 kwa ajili ya kuhudumia jamii katika miradi ya maendeleo kwa mwaka huu hapa nchini.
Akizungumza katika shule ya sekondari Chita halmashauri ya wilaya ya Mlimba, Meneja wa Benki ya NMB kanda ya kati, Nsolo Mlozi alisema benki hiyo kila mwaka imekuwa ikitenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kurejesha faida kwa jamii katika kutoa misaada sekta za afya, elimu na majanga ya asili yanayojitokeza na mwaka huu.
Nsolo alisema kwa mwezi Machi mkoa wa Morogoro imenufaika na misaada katika sekta ya elimu na afya kwa kupata vifaa katika sekta hizo vikiwa na thamani ya sh42.3milioni katika halmashauri tatu za Manispaa ya Morogoro, Malinyi na Mlimba.
Meneja Mahusiano Huduma kwa Serikali Benki ya NMB, Peter Massawe ametaja vifaa hivyo kuwa ni chuo cha Bigwa viti 100 na meza 100, shule ya msingi Sinyaulima Ngerengere vifaa vya ujenzi, Chita sekondari viti 50 na meza 50, Ngoheranga vita 50 na meza 50, shule ya msingi Mwembeni Malinyi madawati 50 na Hospitali ya wilaya Malinyi ikipokea vitanda nane vya kujifungulia akinamama wajawazito.
Kwa upande wa Mkuu wa wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba alisema benki hiyo imekuwa msaada kwa serikali katika kutoa msaada sekta ya afya, elimu kutokana na kuipunguzia mzigo katika kutoa vifaa katika sekta hizo na kuomba taasisi nyingine za kifedha kuiga mfano kwa NMB kurejesha faida wanazopata kwenda katika jamii.