NEWYORK, MAREKANI
MWANAMME mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Matthew Checko (47) amechukua nafasi katika vichwa vya habari nchini Marekani baada ya kuamua kuiba gari la wagonjwa (Ambulance) iliyokuwa imempeleka katika hosptitali iitwayo ‘Mlima Sinai Morningside’ iliyopo Manhattan kwa ajili ya matibabu.
Tovuti ya Daily News ya nchini hapa imesema baada ya Checko kufikishwa hospitalini hapo alitoka kinyemela kisha kuliiba gari hilo lililokuwa limeegeshwa na funguo zikiwa ndani kisha kutokomea nalo.
Taarifa ya Polisi imeeleza tukio hilo lilitokea siku ya Alhamisi, Machi 30, 2023 ambapo gari hilo lilikuwa limeegeshwa nje ya hospitali na halikuwa limefungwa wala hakukuwa na mtu ndani ambapo Checko alitoroka hospitalini saa kumi na moja alfajiri.
Checko alifanikiwa kuingia ndani ya gari hilo akaliendesha umbali wa kilomita zaidi ya 40, wakati polisi walipolifuatilia kupitia GPS, kisha walijaribu kumsimamisha na kulizuia lakini aliwapuuza kwa kupita na mwendao wa kasi.
Polisi waliamua kuweka kifaa ambacho kilitoboa magurudumu ya gari hilo la kubeba wagonjwa na alikamatwa kwa makosa ya ulaghai, kumiliki mali ya wizi, kutoroka Ofisa wa Polisi na kuendesha gari akiwa amelewa.