NAIROBI, KENYA
BALOZI nane chini Kenya zimemsihi kiongozi wa upinzani nchini humo, Raila Odinga aachane na mango wake wa kuhamasisha maandamano kwani unaweza kupelekea machafuko nchini humo.
Balozi hizo nane ikiwemo ubalozi wa Uingereza na Marekani zimeonyesha wasiwasi kuhusu ghasia zinazoanza kushuhudiwa nchini humo kutokana na maandamano hayo ya upinzani.
Takriban watu watatu wameuawa tangu Jumatatu iliyopita wakati upinzani ulipoitisha maandamano ukiitaka serikali kushughulikia kupanda kwa gharama ya maisha. Katika ghasia hizo, raia pia wameibiwa magari kupigwa mawe na biashara kuporwa.
Wakati wa maandamano ya Jumatatu, ilishuhudiwa takribani watu 2000 wakivamia shamba la familia ya rais wa zamani Uhuru Kenyatta. Waliiba mamia ya mifugo, wakachoma sehemu za shamba na kujaribu kutwaa ardhi hiyo. Baadaye kampuni ya mitungi ya gesi inayomilikiwa na familia ya Raila Odinga pia ilishambuliwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kithure Kindiki amesema ghasia hizo zinatishia uthabiti wa nchi na ametoa wito wa kukomeshwa kwa matukio hayo aliyoyataja kama ‘ya kichaa’
Odinga, ambaye alishindwa uchaguzi wa urais mwaka jana na William Ruto, amekataa kukubali matokeo na uamuzi wa mahakama ya juu ambao uliidhinisha ushindi wa Rais Ruto.