NAIROBI, KENYA
MWANASIASA mkongwe nchini Kenya, Raila Odinga, ameendelea kumkomalia Rais wa nchi hiyo, William Ruto kwa kuitisha maandamano yatakayofanyika kila Jumatatu.
Maandamano hayo yalianza jana Jumatatu, Machi 20, 2023 jiji Nairobi na kusababisha baadhi ya maeneo ya jiji hilo kutofanyika shughuli za uchumi ikiwemo biashara.
Maduka,masoko na ofisi zilifungwa jijini humo huku waandamanaji wakiwashambulia kwa mawe polisi waliokuwa wanawatawanya waandamanaji hao kwa mabomu ya machozi na maji yanayowasha.
Maandamano hayo yaliyoanza asubuhi yalichagizwa zaidi ilipofika mchana ambapo Raila Odinga na viongozi wengine wa upinzani waliungana na waandamanaji hao eneo maarufu la biashara liitwalo Eisleigh, jijini Nairobi.
Mara tu baada ya mahakama ya hadhi ya juu nchini Kenya kutupilia mbali kesi aliyoifungua Raila ya kupinga ushindi wa Ruto akidai kuibiwa kura, mwanasiasa huyo alianza kufanya mikutano ya hadhara nchini humo akiueleza umma namna alivyoibiwa kura.
Baadaye mikutano yake ikawa ya kuueleza umma namna serikali ya Ruto ilivyoshindwa kuthibiti kupanda kwa gharama za maisha hususani bei za vyakula na mafuta kupaa.
Raila amewaambia wafuasi wake kuandamana kila Jumatatu hadi Rais Ruto atakapojiuzulu