NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema tafiti zinaonesha kuwa takriban watanzania 5800 hadi 8500 wanahitaji huduma ya kusafisha damu (Dialysisi) au huduma za kupandikizwa figo.
Aidha Waziri Ummy amesema hadi kufikia Januari 31,2023 wagonjwa 3,250 wanapata huduma ya kusafishwa damu na wagonjwa 335 wamepandikizwa figo.
Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Waziri Ummy amesema kati ya wagonjwa hao waliopandikizwa figo, wagonjwa 103 wamepandikizwa hapa nchini katika hospitali mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo waliwapandikiza wagonjwa 10 na Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma walipandikizwa 33.
Amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan inaendelea na utekelezaji wa sera ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inalenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo ugonjwa wa figo kwa umahiri zaidi.
”Huduma za matibabu ya figo hususan za usafishaji wa damu (dialysis)zimekuwa zikitolewa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na Hospitali za Kanda na Hospitali za Rufaa za Mikoa kutoa huduma za dialysis ambapo kwa sasa awamu ya kwanza ya utekelezaji imekamilika ambapo serikali imeanzisha huduma za uchujaji damu kwenye hospitali za mikoa nane kwa kuzipatia mashine 49 za dialysis na kukarabati majengo kwa gharama ya Bilioni 2.8,” amesema na kuongeza.
”Hospitali za Rufaa za Mikoa zilizoanzisha huduma hizi ni za Mtwara, Arusha, Tanga, Kigoma, Kagera, Mara, Iringa na Mwanza ambapo wagonjwa zaidi ya 150 wameweza kufaidika na huduma hizi zinazotolewa na serikali,”amesema.
Akizungumzia awamu ya pili ya upanuzi wa huduma hizo katika hospitali, Waziri Ummy amesema hospitali nyingine 12 zimeanza ambapo mashine za dialysis 110 na za kuchakata maji 11 vimeanza kusimikwa katika Hospitali husika.
“Jumla ya Sh. Bilioni 4.9 zitatumika kujenga vituo vinne vipya vya dialysis kukarabati majengo saba katika Hospitali hizo ni pamoja na Mikoa ya Songea, Morogoro, Mwananyamala, Temeke, Amana, Tumbi, Mawenzi, Chato, Dodoma, AICC Arusha na Mbeya ,”amesema.
Amesema mipango iliyopo ifikapo Desemba 2023, hospitali zote za rufaa nchini zitakuwa zikitoa huduma za usafishaji damu (dialysis) na hivyo kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi, pamoja na kuimairisha huduma za tiba ya magonjwa ya figo nchini.
Pia amesema Serikali imejipanga kuweka jitihada za kipekee ili kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa figo na magonjwa yasiyoambukiza kwa ujumla kwa kuimarisha afua za kinga kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.
”Nawakumbusha umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha kwa kuhimiza ufanyaji wa mazoezi, kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake,kupunguza matumizi ya vilevi,” amesema.