NA DENIS SINKONDE, SONGWE
MKUU wa wilaya ya Momba mkoani Songwe Fakii Lulandala ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kumshikilia kwa saa 48 na kumuhoji Mkuu wa Idara ya Maliasili anayeitwa Joseph Mbogela kwa kosa la kutoa kibali cha kuvuna miti ili kusafisha shamba huku kukiwa na katazo la kuvuna miti lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mwaka 2022.
Dc Lulandala ametoa agizo hilo Machi 9,2023 wakati akipita katika eneo la Chigambo Kijiji cha Ikana alipomkuta Daniel Simbeye mkulima wa eneo hilo na Mkazi wa Jiji la Mbeya akijiandaa kuvuna miti katika eneo la hekari 12 ambazo amedai analimiliki kihalali na ana kibali kinachomruhusu kuvuna miti hiyo kilichotolewa na idara ya Misitu na Maliasili Wilaya ya Momba.
Dc Lulandala ameliagiza Jeshi Hilo kumshikilia Mbogela kwa kosa la Kuhatarisha usalama wa Misitu na kutoa kibali kinyume na utaratibu wa utoaji wa vibali hivyo unaomtaka Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama kuidhinisha kibali hicha ambacho yeye hakushirikishwa katika mchakato wa utoaji.
Aidha Lulandala amemsimamisha Mkulima huyo kuendelea na shughuli za ufyekaji wa Miti mpaka kamati ya ulinzi na usalama itakavyoshauri katika Usafishaji wa shamba hilo.
Dc Lulandala ametoa onyo kwa watumishi wote wa Idara ya Maliasili wilayani humo kufuata taratibu katika utendaji wao wa kazi na kuacha mara moja kutoa vibali vya uvunaji wa miti hadi katazo la Mkuu wa Mkoa litakapotenguliwa na kuelekeza vinginevyo ili kulinda Misitu ya yote ya asili iliyopo Mkoani Songwe.